1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Annan haoni dalili njema kwa mkwamo wa sasa wa mzozo wa Zimbabwe

Mohmed Dahman21 Oktoba 2008

Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe kimesema leo hii kwamba ni uchaguzi mpya tu ndio utakaoweza kutatuwa mzozo juu ya nani anayepaswa kudhibiti nyadhifa muhimu za mawaziri.

https://p.dw.com/p/FeJP
Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.Picha: AP

Suala hilo limekua la kuamuwa mbichi au mbivu katika makubaliano ya kugawana madaraka yaliotiwa saini kati ya upinzani na Rais Robert Mugabe.

Mugabe na Tsvangirai kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC wamekuwa wakilumbana kuhusiana na udhibiti wa wizara na mazungumzo yao ya ana kwa ana ya wiki kadhaa yameshindwa kutanzuwa mkwamo huo.

Mkwamo huo wa kisiasa umezusha hofu kwamba makubaliano ya kugawana madaraka yaliofikiwa mwezi uliopita yumkini yakasambaratika na kuutumbukiza uchumi wa Zimbabwe kwenye matatizo zaidi.

Msemaji wa MDC Nelson Chamisa amesema kigezo wanachopendelea ni kukamilisha mazungumzo hayo lakini ikishindikana kufikiwa kwa makubaliano wananchi wa Zimabawe watakuwa hawana chaguo jengine isipokuwa kuamuwa nani anayestahiki madaraka kwa kupitia uchaguzi ambao utakuwa wa kuaminika.

Tsvangirai alimshinda Mugabe katika uchaguzi wa rais hapo tarehe 29 mwezi wa Machi lakini kwa kura chache zilizoshindwa kuepusha marudio ya uchaguzi hapo mwezi wa Juni ambao Mugabe alishinda bila ya kupingwa baada ya Tsvangirai kujitowa kwa kusema kwamba wafuasi wake walikuwa wakitendewa vitendo vya ukatili na kutishwa.

Chamisa amesema kumekuwepo kutokuaminiana kati ya chama cha Mugabe cha ZANU- PF na kile cha MDC kulikojionyesha katika hatua ya serikali kushindwa kumpatia Tsvangirai paspoti mpya baada ya ile ya zamani kujaa miezi kadhaa iliopita.

Tsvangirai ameshindwa kuhudhuria mkutano wa viongozi wa kanda nchini Swaziland hapo jana baada ya serikali kumpatia tu hati za kusafiri za dharura.

Kwa maoni ya Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan hali hiyo haitowi ishara njema.

Anasema ni vigumu sana kuachilia madaraka unapokuwa nayo kwa muda mrefu na anafikiri kilicho muhimu ni kwamba hata kama unakuwa na makubaliano unafikiri yanaweza kufanya kazi na wawekezaji wenye imani? Amesema jambo hilo kwa kweli litategemea viongozi hao wawili na kwamba Rais Mugabe anaweza kujitolea kwa mengi na inabidi aonyeshe ukarimu kwa kuitanguliza mbele nchi yake.

Annan anafikiri iwapo watu hao wawili watashirikiaana wataweza kubadili hali ya nchi hiyo na iwapo kuna mmoja anayesita sita au hataki kushirikiana na kugawana madaraka kikamilifu hapo tena kutakuwa na tatizo.Na kuanzia hivi leo haoni kama kuna dalili njema.Hata hivyo amesema hakuna ajuaye watu hubadilika.

Mkutano wa Swaziland ulioitishwa hapo jana na Jumuiya ya Ushrikiano wa Maendeleo ya nchi wanachama 15 za kusini mwa Afrika SADC kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo katika juhudi za kuunda baraza la mawaziri la pamoja umeahirishwa hadi tarehe 27 mwezi wa Oktoba na utafanyika mjini Harare Zimbabwe.

Tsvangirai amekuwa akikishutumu chama cha ZANU- PF ambacho kilishindwa katika uchaguzi wa bunge hapo mwezi wa Machi kwa kujaribu kujinyakulia takriban wizara zote muhimu na kuiwachia MDC dhima ya mshirika ndogo katika serikali mpya.