Annan kwenda Syria haraka
28 Mei 2012Mauaji ya kinyama ya zaidi ya watu 100 nchini Syria yanaweza kuwa ni mwanzo wa kuwaweka katika njia panda rais Bashar al-Assad na mpatanishi wa kimataifa Kofi Annan. Wanadiplomasia wanasema ishara sio nzuri kwa juhudi za kila upande.
Baraza la usalama la umoja wa mataifa jana lilishutumu vikali kuhusika kwa serikali ya Syria katika mashambulizi ya makombora dhidi ya kijiji cha Houla . Taarifa yake hata hivyo haikuweza kuyaleta mataifa makubwa duniani pamoja katika azma ya kufikisha mwisho mzozo huo.
Marekani yashutumu
Marekani na mataifa ya Ulaya , wamesema kuwa mauaji hayo ni ishara mpya ya jinsi utawala wa Assad ulivyo wa kinyama. Ushahidi ni wazi na kuna ishara kamili ya uhusika wa serikali katika mauaji haya, amesema Peter Wittig , balozi wa Ujerumani katika umoja wa mataifa.
Urusi inapinga ushahidi huo na kuendelea kuikingia kifua nchi hiyo mshirika wake wa karibu katika mashariki ya kati.
Hatuamini kuwa serikali ya Syria itapendelea kuharibu ziara ya mjumbe maalum Kofi Annan , ziara ambayo ni muhimu sana ambapo tunatarajia mengi ya maendeleo, amesema Igor Pankin, naibu balozi wa Urusi katika umoja wa mataifa.
Urusi yalaumu waasi
Urusi na serikali ya Syria zinaendelea kuyalaumu makundi ya upinzani pamoja na watu kutoka nje wenye misimamo mikali kwa kuleta ghasia nchini humo. Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague amesema kuwa hii ni mbinu ya muda mrefu sasa ya serikali ya Syria.
"Hii ni mbinu inayofahamika ya utawala wa Assad ya kuwalaumu watu wengine kwa kile kinachotokea nchini mwake, ili kujaribu kujitoa katika wajibu kwa kiwango cha mauaji na uharibifu. Tumechukizwa sana katika serikali ya Uingereza na katika jumuiya ya kimataifa kwa kile tulichokiona katika muda wa siku chache zilizopita, hususan vifo vya zaidi ya watu 100 ambao hawakujihami kwa silaha , wanaume, wanawake na watoto".
Jeshi huru la Syria pamoja na waasi wengine wakati huo huo wanasema kuwa mauaji ya Houla ni sababu nyingine kwanini hawataheshimu kusitisha mapigano ambayo yamepatanishwa na Kofi Annan lakini ambayo hayajafanyakazi.
Wataalamu wa mataifa ya magharibi wanasema kuwa Assad huenda ataendelea kuwapo madarakani kwa miezi kadha, kama sio muda mrefu zaidi. Wakati waangalizi wa makubaliano ya kusitisha mapigano wa umoja wa mataifa nchini Syria , tayari wanashambuliwa na ghasia zinaongezeka , kuna matumaini finyu ya juhudi za amani za Kofi Annan .
Mauaji ya kuchukiza
Mkuu wa ujumbe wa umoja wa mataifa nchini Syria meja jenerali Robert Mood amesema kuwa mauaji hayo ni ya kuchukiza.
"Haisameheki . Vifo vya watoto zaidi ya 50, hali ya baadaye ya Syria , ni kitu ambacho kinasikitisha sana".
Mpango wa Annan haujakufa, amesema balozi wa Uingereza katika umoja wa mataifa Mark Lyall Grant. Lakini katika mazungumzo kuhusu mashariki ya kati kesho Jumanne na Syria siku ya jumatano baraza linahitajika kuwa na mkakati maalum wa majadiliano juu ya mpango wa Annan na kile baraza hilo la amani linaloweza kufanya kumsaidia mjumbe huyo mpango wake kufanyakazi.
Wakati huo huo kundi la wapinzani limesema leo kuwa mashambulio ya jeshi la serikali ya Syria yamesababisha mauaji ya watu 41 katika mji wa Hama katika muda wa saa 24 zilizopita.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe /rtre
Mhariri: Hamidou Oummilkheir