Antony Blinken na Rutte wa NATO wakutana kuhusu vita Ukraine
13 Novemba 2024Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amekutana na katibu mkuu wa NATO Mark Rutte, mjini Brussels, wakati ambapo utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden unaomaliza muda wake ukitaka kuimarisha misaada kwa ajili Ukraine kabla ya kurejea kwa Donald Trump kwenye ikulu ya Marekani.
Kulingana na Blinken, pia alijadili na mkuu wa NATO Mark Rutte, juu ya vikosi vya Korea Kaskazini vilivyoingizwa vitani na Urusi.
Blinken ameongeza kuwa vikosi hivyo vinahitaji kujibiwa vikali.
"Hatua ya kuongezeka kwa vikosi vya Korea Kaskazini katika mapigano kunahitaji jibu thabiti. Hivyo basi ni muhimu kwetu kutafuta njia za kushirikiana kwa undani zaidi.”
Marekani ina wasiwasi juu ya kile ambacho Urusi inaweza kufanya ili kuyaimarisha majeshi ya Korea Kaskazini, ikiwa ni pamoja na uwezo wao wa kinyuklia.
Marekani imesema wanajeshi wa Korea Kaskazini wamekuwa wakishirikiana katika mapigano na vikosi vya Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine.
Wakati huo huo, Blinken ameitaka Israel itekeleze hatua za kweli na za muda mrefu za kusimamisha mapigano kwenye Ukanda wa Gaza ili kuruhusu utoaji wa misaada kwa wakaazi wa eneo hilo walioathiriwa na vita.
Blinken amesema hatua hizo zinahitajika katika maeneo makubwa ya Ukanda wa Gaza.
Blinken pia amewaambia waandishi habari mjini Brussels kwamba Israel inachukua hatua ili kuishughulikia hali mbaya inayowakabili watu kwenye maeneo ya wapalestina.