1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria ngumu zaidi kuhusu udhibiti wa Jerusalem yapitishwa

Mjahida 2 Januari 2018

Bunge la Israel limepitisha sheria inayonuiwa kuifanya hali kuwa ngumu kwa serikali hiyo kuikabidhi Palestina sehemu ya Jerusalem iwapo watawajibika kufanya hivyo kufuatia mpango wowote wa amani katika siku za usoni.

https://p.dw.com/p/2qExC
Israel Jerusalem Panorama
Picha: Reuters/R. Zvulun

Sheria hiyo iliyowasilishwa na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia iliyopitishwa kwa kura 64 dhidi ya 51 ni pigo la hivi karibuni kwa matumaini yaliyokuwepo kwa suluhu ya mataifa hayo mawili likija suala la mgogoro kati ya Israel na Palestina.

Msuada huu uliyoanzishwa na Shuli Moalem-Refaeli wa chama cha mrengo wa kulia, unakuja wiki kadhaa baada ya uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, hali iliyozua maandamano makubwa katika maeneo ya Palestina. 

Sheria hiyo hairuhusu serikali ya Israel kutoa ardhi inayofikiriwa na nchi hiyo kuwa sehemu ya Jerusalem, bila ya idhini ya bunge.

Yani hoja hiyo inabiddi ipitishwe kwa theluthi mbili ya kura zitakazopigwa bungeni hii ikimanisha kura 80 badala ya 61 kati ya wanachama 120 wa bunge hilo.

Aidha wanasiasa wa chama hicho cha mrengo wa kulia nchini Israel wamezungumzia kwa pamoja kuvunja maeneo ya wapalestina katika mji wa Jerusalem ili kuongeza udhibiti wa maeneo yanayokaliwa na wayahudi.

Israel Siedlungspolitik Abstimmung im Parlament
Bunge la IsraelPicha: Reuters/A. Awad

Palestina yasema sheria hiyo ni njia moja ya Israel kutangaza vita vya wazi na mamlaka yake.

Israel ilichukua udhibiti wa Mashariki mwa mji huo na eneo la ukingo wa Magharibi mnamo mwaka 1967, baadaye ikaiunganisha Jerusalem Mashariki na taifa lake jambo ambalo halikuwahi kutambuliwa na jamii ya Kimataifa.

Hata hivyo Nabil Abu Rdainah msemaji wa rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmood Abbas ameikosoa sheria hiyo huku akisema kura hiyo inaonyesha wazi kwamba Israel imetangaza rasmi kumalizika kwa juhudi za kuleta Amani. Ameongeza kuwa kupitishwa kwa sheria hiyo ni kutangaza vita dhidi ya watu wa Palestina.

Israel imekuwa ikiungangania mji wa Jerusalem kama mji wake usiogawika huku wapalestina wakitaka Mashariki ya Jerusalem kama mji mkuu wa dola lao la siku za usoni.

Huku hayo yakiarifiwa ndege za kivita za Israel zimeyashambulia maeneo ya Hamas mjini Gaza mapema hii leo ikiwa ni majibu ya kombora lililorushwa kutoka Palestina lililolenga Kusini mwa Israel. Takriban wapalestina 13 wameuwawa tangu tangazo hilo la kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Isarel.  

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP/dpa/Reuters

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman