1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Argentina yachunguza madai dhidi ya Mohammed bin Salman

28 Novemba 2018

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu, Human Rights Watch limesema kwamba mamlaka za kisheria nchini Argentina zinatathmini ombi la kutaka Mohammed bin Salman achunguzwe kufuatia mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi

https://p.dw.com/p/38xye
Saudi Arabien Mohammed bin Salman
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

Human Rights Watch imesema uchunguzi huo unafaa kufanywa nchini Argentina, ambapo bin Salman anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa G20 wiki ijayo mjini Buenos Aires, kwa madai ya kuhusishwa na mauaji hayo pamoja na uhalifu wa kivita uliotekelezwa na muungano unaoongozwa na Saudi nchini Yemen. 

Gazeti la Clarin limeleeza kwamba Jaji Ariel Lijo amewaagiza wakuu wa mashtaka kubaini iwapo Mrithi huyo wa Ufalme anaweza kufunguliwa mashtaka nchini Argentina kufuatia mauaji hayo.Human Rights Watch pia imesema katiba ya Argentina inatambua mamlaka ya ulimwengu kwa uhalifu na mateso, kwa maana kwamba taifa hilo linaweza kusikiliza mashtaka ya uhalifu bila kujali uraian wa wahusika au mahali uhalifu huo ulipotekelezwa.

Mkuu wa  Human Rights Watch Kenneth Roth limesema hatua ya Mohammed bin Salman kuhudhuria mkutano huo wa G20 mjini Buenos Aires inaweza kuzifanya mahakama za Argentina kuwa kituo cha kuwasaidia waathiriwa wa uhalifu ambayo wanashindwa kutafuta haki nchini Yemen na Saudi Arabia.

Tunesien Proteste gegen Besuch Saudi Kronprinz Mohammed bin Salman
Picha: Getty Images/AFP/F. Belaid

Hayo yanajiri huku maandamano ya wanahabari na mashirika ya kijamii yakitarajiwa kuendelea leo nchini Tunisi kupinga ziara ya bin Salman nchini humo leo. Maandamano hayo yalianza jana katika miji ya Tunis na Sfax.

Mmoja wa waandishi habari Soukaina Abdessamad amesema kwamba mapinduzi ya Tunisia hayawezi kukubali kumpokea bin Salman na kumruhusu kujitakasa na mauaji kupitia ziara yake. Soukaina amesema,´Chama cha wanahabari nchini Tunisia ni sehemu ya mashirika ya kijamii, tulitaka kukusanyika na kuonyesha umoja wetu katika kupinga ziara ya bin Salman. Tulitaka kuungana chini ya kauli mbiu'hatukubali Tunisia iharibiwe,´ ili sote tukatae Tunisia kutumiwa  kama nchi ambako  utata unaweza kupuuzwa.

Tangu uasi wa umma mwaka 2011 yaliyofikisha kikomo uongozi wa Ben Ali na kusababisha vuguvugu ka mabadiliko katika nhi za Kiarabu yaliyochangia msukosuko wa mataifa hayo, Tunisia ndio pekee miongoni mwa mataifa machache ya kiarabu ambapo maandamano yanaruhusiwa. Saudi Arabia imesema kwamba Mohammed bin Salman hakufahamu kuhusu mauaji ya Khashoggi yaliyofanywa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul Uturuki.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/DPAE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman