1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Armenia, Azerbaijan zakubaliana kumaliza vita

10 Novemba 2020

Armenia na Azerbaijan zimetangaza mapema leo makubaliano ya kusitisha mapigano kuhusu mkoa wa Nagorno-Karabakh ulioko Azerbaijan chini ya muafaka uliotiwa saini na Urusi

https://p.dw.com/p/3l5BU
Aserbaidschan-Armenien | Konflikt in Berg-Karabach
Picha: Iliya Pitalev/Sputnik/dpa/picture alliance

Wanajeshi wa kulinda amani wa Urusi wamepelekwa mapema leo katika mkoa ulioharibiwa kwa vita wa Nagorno-Karabakh kama sehemu ya mpango wa kusitisha mapigano ambao Rais Vladmir Putin amesema utasafisha njia ya kupatikana suluhisho la kudumu la kisiasa kwa mgogoro wa eneo hilo.

Soma pia:Makubaliano mapya yatangazwa Nagorno-Karabakh

Mpango huo, uliosainiwa na Armenia, Azerbaijan na Urusi, ulioanza kutekelezwa usiku wa manane jana umefuatia mgogoro uliowauwa maelfu ya watu, kusababisha wengi kupoteza makazi na kutishia kuitumbukiza kanda hiyo nzima katika vita.

Chini ya mkataba huo, Azerbaijan itayadhibiti maeneo yote iliyoyakamata, ukiwemo mji wa pili kwa ukubwa wa mkoa huo, Shusha, nao wanajeshi wa Kiarmenia wasalimishe udhibiti wa maeneo mengine kadhaa kati ya sasa na Desemba mosi.

Konflikt in Berg-Karabach
Jeshi la Azerbaijan liliukamata mji wa ShushiPicha: Azerbaijani Ministry Of Defence/TASS/dpa/picture alliance

Putin amesema watu waliokimbia makazi yao watarudi Nagorno-Karabakh, kutakuwa na mabadilishano ya wafungwa wa kivita na waliouawa na shughuli za kiuchumi na usafiri katika eneo hilo zitafunguliwa tena kwa msaada wa walinzi wa mpakani wa Urusi. "Tutasonga mbele kutokana na msingi kuwa makubaliano yaliyofikiwa yataunda mazingira mwafaka ya kupatikana suluhisho la muda mrefu na pana la mzozo kuhusu Nagorno-Karabakh kwa msingi wa haki, na katika maslahi ya watu wa Armenia na Azerbaijan."

Walinda amani wa Urusi watabaki eneo hilo kwa karibu miaka mitano. Watawekwa katika uwanja wa mapambano katika wa Nagorno-Karabakh na ukanda wa kati ya eneo hilo na Armenia. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema imeanza kuwapeleka askari 1,960, pamoja na vifaa na magari.

Soma pia: Armenia, Azerbaijan zalaumiana kukiuka makubaliano ya amani

Machafuko Armenia

Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev amesema Uturuki pia itahusika katika juhudi za kulinda Amani. Hakujatolewa kauli yoyote ya haraka kutoka Ankara. Uturuki ni muungaji mkono mkubwa wa Azerbaijan wakati Urusi ina mkataba wa ulinzi na Armenia na ina kituo cha kijeshi nchini humo. Nchini Armenia, Waziri Mkuu Nikol Pashinyan alijaribu kuweka sura ya ujasiri kuhusu hali hiyo. "Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na uchunguzi wa hali ya kijeshi na kwa kuzingatia tathmini ya watu walio na ufahamu wa kutosha kuhusu hali ya kijeshi. Tunapaswa kuelewa jeshi letu lilipigana dhidi ya magaidi, jeshi la pili la NATO yaani Uturuki na jeshi la Azerbaijan."

Vurugu zilizuka mapema leo bungeni wakati waandamanaji walipouvamia ukumbi wa vikao wakiupinga mpango huo uliotangazwa na Pashanyian wakimtaka ajiuzulu. Awali, maelfu ya waandamanaji walikusanyika nje ya majengo ya serikali mjini Yerevan, na kuvamia ofisi mbalimbali huku wakipekua na kuvunja madirisha. Ripoti za ndani zinasema spika wa bunge Ararat Mirzoyan alivamiwa na kuchapwa.

Reuters, AFP, DPA, AP