Armenia, Azerbaijan zakubaliana kuendeleza mpango wa amani
23 Mei 2022Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, alikutana na kila upande kwa wakati wake siku ya Jumapili (Mei 22) mjini Brussels, baada ya Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan na Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Pashinyan, kukutana na kukubaliana juu ya umuhimu wa kuendeleza mpango wa amani, kwa mujibu wa Michel.
Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo inasema viongozi hao walikubaliana kuendeleza majadiliano kwa ajili ya mkataba rasmi wa amani siku zijazo, ambao utasimamia mahusiano kati ya Armenia na Azebaijan.
Kwa mujibu wa Michel, mawaziri wa mambo ya nje watakutana katika wiki za hivi karibuni kuratibu muendelezo wa majadiliano na marais hao watatu watakutana baina ya Julai na Agosti.
Juhudi za pamoja zaanzishwa
Aliyev na Pashinyan walikubaliana pia kuwa na kamisheni ya pamoja ya usimamizi wa mpaka na usalama wake ambayo itaanza kazi siku chache kutoka sasa, na pia kwa pamoja watahakikisha vikwazo vya usafiri na usafirishaji baina ya mataifa hayo vinaondoshwa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya rais wa Azerbaijan, Aliyev alimuambia Michel kwamba nchi yake ilishaweka masharti matano yanayokwendana na sheria za kimataifa juu ya kurejesha mahusiano kati yake na Armenia na kusaini makubaliano ya kudumu ya amani.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Armenia alijadiliana na Michel juu ya hali ya kibinaadamu kwenye jimbo la Nagorno-Karabakh, na kusisitiza umuhimu wa kuitatuwa, kwa mujibu wa ofisi yake.
Shinikizo dhidi ya Pashniyan
Hata hivyo, Pashniyan anakabiliwa nashinikizo kubwanchini kwake kutoka kwa wapinzani wa mpango huo wa amani, wanaodai kwamba aliongoza vibaya wakati wa vita vya mwaka 2020, na kwamba kauli zake za karibuni zinamaanisha kuwa anaridhia sana matakwa ya Azerbaijan.
Katika wiki za hivi karibuni, waziri mkuu huyo amekuwa akikabiliwa na wimbi la maandamano katika mji mkuu, Yerevan, tangu aliposema kuwa jumuiya ya kimataifa inaitaka Armenia kushusha madai yake kwenye jimbo la Nagorno-Karabakh.
Maandamano hayo yamesadifiana pia na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, ambao umeyafanya mataifa yaliyowahi kuwa sehemu ya Muungano wa Sovieti kuhakiki upya usalama wao wenyewe, wakati Moscow ikijikita kwenye makabaliano makubwa kabisa na mataifa ya Magharibi baada ya miongo kadhaa ya amani baina yao.
Mnamo mwaka 2020, Armenia na Azerbaijan zilipigana kwa wiki sita mfululizo wakiwania udhibiti wa jimbo la Nagorno-Karabakh, ambalo kijiografia ni sehemu ya Azerbaijan lakini kijamii linakaliwa na watu wenye asili ya Armenia.
Katika vita hivyo, vikosi vya Azerbaijan viliwafurusha wanajeshi wa Armenia kutoka maeneo makubwa waliyokuwa wakiyakalia tangu miaka ya 1990, kabla ya Urusi kuingilia kati na kupatanisha pande hizo mbili.