1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asasi za kiraia zatoa wito kuachiwa mashekhe Tanzania

George Njogopa15 Machi 2023

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Tanzania yametoa wito kwa serikali yakitaka masheikh wanaondelea kushikiliwa magerezani kwa tuhuma za ugaidi kuachiwa mara moja au wapatiwe haki ya kujitetea mahakamani.

https://p.dw.com/p/4Oj4P
Tansania Daressalam | State House | Samia Suluhu Hassan, Präsidentin
Picha: Ericky Boniphace/DW

Hatua hiyo inakuja baada ya sheikh mmoja aliyekuwa akishikiliwa katika gereza  jijini Dar es salaam kufariki dunia huku familia yake ikihoji  mazingira ya kifo chake.

Katika taarifa yao ya pamoja mashirika hayo yameonyesha kutilia shaka mwenendo wa mashtaka yanayowakabili wakidai wamesota rumande kwa miaka mingi huku kesi zao zikishindwa kusikikizwa mahakamani.

Kuhusiana na suala hilo la kukaa gerezani kwa kipindi kirefu zaidi, kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania, , kinaamini hali hiyo ni kubinya haki za binadamu na kuzorotesha usawa wa haki jinai.

Soma pia:Tume ya Afrika ya haki za binadamu ziarani Tanzania

Mkurugenzi wake mkuu, Anna Henga mbali ya kutaka mamlaka zinazoshughulia suala hilo kufumbua macho, amehimiza kufanyika uchunguzi huru.

akienda mbali katika hilo ametaka uchunguzi utakaomulika mazingira yaliyosabisha kifo  cha sheikh Said Mohammed Ulature aliyekuwa akishikiliwa katika gereza la Ukonga.

Magereza:Shekhe alifariki kwa shinikizo la damu

Mamlaka katika gereza hilo la Ukonga zinasema sheikh huyo aliyesota rumande kwa zaidi ya miaka 7 alifariki dunia kutokana na shinikizo la damu.

Alikuwa miongoni mwa masheik kadhaa waliokamatwa wakihusishwa na mashtaka ya ugaidi.

Soma pia:Asasi za kiraia kutoridhishwa na tathmini kuhusu Loliondo

Kuendelea kusota kwao rumande kwa kipindi chote hicho kumezidi kuchochea miito ya kutaka waachiliwe huru au kifikishwa mahakamani  kujibu mashtaka yao.

Akiwa sehemu ya tamko hilo la leo la mashirika ya kutetea haki za binadamu, Katibu wa Jumuiya na Tasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema, haki bado ni changamoto.

Kauli ya Rais Samia wa Tanzania yazusha mjadala

Ponda ambae nae amekumbana na panda shuka chungumzima katika harakati zake za kutetea haki amewaambia waandishi wa habari kwamba,bado mfumo wa haki jinai  ni kitendawili kinachoendelea kuwaandama wengi.

Tamko hilo la watetezi wa haki za binadamu linakuja katika wakati ambapo tume ya haki jinaiiliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni ikiendelea na kazi maalumu ya ukusanyaji maoni kuhusu uboreshwaji wa mifumo ya haki jinai.

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa makundi mbalimbali wanaonyoosha kidole juu ya ndugu na jamaa zao kuendelea kusota mahubusu kwa kipindi kirefu bila kufikishwa mahakamani.