1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asif Ali Zardari achaguliwa rais mpya wa Pakistan

Saumu Mwasimba6 Septemba 2008

Wafuasi wa chama cha PPP wautaja ushindi huo kuwa ushindi wa Demokrasia Pakistan

https://p.dw.com/p/FCcC
Asif Ali ZardariPicha: AP

Kiongozi wa chama cha Pakistan Peoples Party PPP Asif Ali Zardari amethibitishwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika katika mabunge ya taifa na mikoa nchini Pakistan.

Zardari anachukua wadhifa huo baada ya kujiuzulu madarakani Pervez Musharraf kutokana na shinikizo za kitisho cha kuondolewa madarakani na kushtakiwa.

Zardari amechaguliwa kwa kura 481 zilizopigwa kwa njia ya siri kati ya kura zote 702. waziri wa habari Sherry Rehman ameutaja ushindi huo wa Zardari kuwa ni ushindi wa kidemokrasi na kuongeza kwamba rais mteule ameahidi kuwa tayari kuimarisha mfumo wa bunge ili kufikia malengo ya taifa.

Chama cha waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif cha PML-N kimekubali kushindwa kikisema kwamba kinamatumaini kwamba Zardari atajiuzulu katika wadhifa wa kuwa kiongozi wa chama chake na kubakia na uongozi wa taifa.

Zardari ameshinda uchaguzi huo dhidi ya wapinzani wake, SaeedUzzaman Siddiqui jaji wa zamani aliyegombea kwa tikiti ya chama cha waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharrif na Mushahid Hussain Sayed afisa wa ngazi ya juu wa kilichokuwa chama tawala nchini humo chini ya Musharraf.

Zardari na changamoto ya matatizo makubwa ya kiuchumi pamoja na mapambano ya wanamgambo wakiislamu yanayotishia usalama nchini humo.

Mapema hii leo zaidi ya watu wanne waliuwawa na wengine 30 wakajeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea kwenye kituo cha ukaguzi wa polisi nje ya mji wa kaskazini magharibi wa Peshawar.

Kundi lenye mafungamano na Al Qaeda nchini humo limekuwa likihusika mara nyingi na mashambulio ya mabomu nchini Pakistan na zaidi katika eneo hilo la kaskazini magharibi na kulenga vikosi vya usalama.