Asilimia 25 ya Commerzbank ya Ujerumani ni mali ya serekali
9 Januari 2009Kutokana na mbinyo wa mzozo wa kiuchumi duniani, serekali ya Ujerumani imeamuwa kushiriki moja kwa moja katika benki ya kibinafsi, ya pili kabisa kwa ukubwa hapa nchini, Commerzbank. Serekali imeingiza Euro bilioni kumi katika benki hiyo kuhakikisha kwamba benki hiyo inainunuwa benki ya Dresner, ambayo ni tawi la shirika kubwa la bima la Allianz. Hivyo, serekali sasa itamiliki asilimia 25 ya benki hiyo pamoja na hisa moja zaidi. Serekali ya Shirikisho pia itakuwa na usemi kuhusu maamuzi muhimu yatakayochukuliwa na mkutano mkuu wa benki hiyo.
Pale habari hiyo mpya ilipojulikana jana, wafanya kazi wengi katika eneo lililo na majengo ya mabenki mjini Frankfurt walikuwa wameshatoka makazini. Kila mmoja wao alikuwa na maoni yake. Wako waliosema kwamba hawajashtushwa na hatua hiyo, kwa vile katika siku chache zilizopita kumetolewa sura mbali mbali juu ya hali ilivyo kuhusiana na kuchanganyishwa Dresner Bank na Commerzbank. Wako waliolalamika kwamba kila wakati waliarifiwa kwamba kuchukuliwa benki ya Dresner na benki ya Commerz kulikuwa karibu kumemalizika. Kwa wafanya kazi wa Commerzbank walio wazee, hamna athari kubwa zitakazowapata, lakini kwa wale walio vijana, bila ya shaka, wana hofu. Wengi wao watafurahi angalau kubakia na ajira zao.
Matatizo yalikuweko katika kununuliwa Dresner Bank na Commerzbank. Magazeti yaliandika kwamba baada ya benki hizo mbili kuchanganyika, taasisi mpya iliochomoza , bado ikibakia na jina la Commerzebank, haijaweza kubakia na asilimia nane ya mtaji wake. Hivi sasa benki hiyo imeomba ipatiwe msaada kutoka ule mfuko maalum wa serekali wa kuleta utulivu katika masoko ya fedha pamoja na mtaji wa ziyada wa Euro bilioni 10. Na badala yake serekali itamiliki asilimia 25 ya benki hiyo pamoja na hisa moja. Mkuu wa Commerbank, Martin Blessing, amesema.
"Bila ya shaka, katika robo ya mwisho ya mwaka uliopita tumejionea malalamiko makubwa sana kuhusu masoko ya fedha. Sisi tunataka kuendelea kama Commerzbank, na pia baada ya kuichukuwa Dresner Bank, kujenga na kuwa benki yenye nguvu sana hapa Ujerumani. Na kwa maslaha ya utulivu, tumeamuwa kuichukuwa hatua hiyo."
Mwezi Novemba mwaka jana. Commerzbank ilipatiwa Euro bilioni nane kutoka ule mfumo wa kutuliza masoko ya taasisi za fedha. Hata hivyo, benki hiyo ilitaka kuichukuwa kabisa Dresner Bank. Bwana Blessing alisema wateja inawabidi wasiwe na wasiwasi, na kwamba benki hiyo itegemewe katika kuyapa mikopo makampuni. Serekali ya Ujerumani ilikuwa na wasiwasi sana kwamba kunaweza kuwepo mkwamo katika utoaji wa mikopo, na ndio maana ikachukuwa hatua hii ya sasa. Waziri wa uchumi, Michael Glos, anaonekana amepumua:
" Sasa ni wazi kwamba tutaendelea kuwa na benki kubwa itakayoweza kutoa huduma, benki ambayo itakuwa zaidi katika hali ya kutoa mikopo ya kuzalisha bidhaa kwa ajili ya uchumi. Na kuna uwezekano kwamba kwa vile serekali ya shirikisho ina sehemu katika benki hiyo, masoko yataweza kupata fedha kwa bei nzuri zaidi kuliko vile ingekuwa hali vingine."
Pia rais na mkuu wa bodi ya usimamizi ya Commerzbank, Klaus-Peter Müller, ameukaribisha msaada huo wa kutoka serekalini, hivyo benki hiyo sasa ina zana kuweza kushindana duniani. Hasa sasa inaweza kuwa muhimu zaidi kwa wafanya biashara wa wastani.
Sasa serekali itabidi iuangalie uchapaji kazi wa mameneja wa Commerzbank. Sasa serekali ya shirikisho itakuwa na kauli ya mwisho katika maaamuzi ya mkutano mkuu wa wenye hisa katika benki hiyo,na pia kuwa na usemi katika maamuzi muhimu.