1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Askari 29 wa Niger wauwawa kwenye shambulizi la itikadi kali

4 Oktoba 2023

Utawala wa kijeshi nchini Niger umesema wanajeshi wake 29 wameuwawa katika shambulizi lililofanywa na makundi ya itikadi kali karibu na mpaka wa taifa hilo na Mali.

https://p.dw.com/p/4X6V3
Mwanajeshi akishika doria katika eneo la Almoustarat
Mwanajeshi akishika doria katika eneo la AlmoustaratPicha: Sebastien Rieussec/Hans Lucas/IMAGO

Waziri wa Ulinzi wa Niger Luteni Jenerali Salifou Mody amesema zaidi ya wapiganaji 100 wanaotumia mabomu ya kuundwa kienyeji wamekuwa wakiwalenga walinzi wa usalama wa taifa hilo wanaoshika doria na ulinzi wa mpakani.

Kufuatia vifo hivyo, utawala wa kijeshi ambao umechukua madaraka baada ya mapinduzi ya Julai dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia umetangaza siku tatu za maombolezo.

Hili ni shambulio la pili lililowalenga wanajeshi wa Niger kwa juma hili pekee.

Hata hivyo Mody alionesha ishara ya hali kuwa imedhibitiwa na kwamba jeshi la Niger lilimudu kuharibu nyenzo za vita za wanamgambo ikiwemo magari 15 na kukamata shehena ya silaha.