1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad akana kuhusika na mauaji ya Houla

4 Juni 2012

Rais Bashar Assad wa Syria ameutetea ukandamizaji wa jeshi lake dhidi ya wapinzani, akisema kwamba daktari anayefanya operesheni ya dharura hawezi kuambiwa ana damu mikononi mwake kwa kujaribu kuyaokoa maisha.

https://p.dw.com/p/157P6
Rais Bashar al-Assad wa Syria.
Rais Bashar al-Assad wa Syria.Picha: AP

Kauli ya Assad kukana mauaji ya Houla inakuja wakati mjumbe wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan, akitaka mpano wake wa amani uhakikiwe upya, naye Rais Vladimie Putin akijitayarisha kuzungumza na viongozi wa Umoja wa Ulaya, ambapo suala la Syria linatazamiwa kutawala ajenda ya mazungumzo hayo.

Katika hotuba yake ya mwanzo tangu mwezi Januari, Rais Assad ameonekana kutokutikiswa na lawama za kimataifa kwake kwa namna jeshi lake linavyokabiliana na miezi 15 ya upinzani dhidi yake, na ambako kumesababisha vifo vya watu 13,000 hadi sasa kwa mujibu wa makundi ya wanaharakati.

Rais huyo amekataa kabisa kuhusika kwa jeshi lake na mauaji ya maangamizi ya Houla, ambayo yalipelekea vifo vya zaidi ya watu 100, wengi wao wanawake na watoto, akisema kwamba hata wanyama wasingefanya ukatili kama huo.

"Hata mnyama asingeliweza kukifanya kile ambacho tumekiona. Hakuna njia ya kukielezea kitu hicho, si kwa lugha ya Kiarabu wala lugha nyengine yoyote. Kila tukikumbuka jambo hili, sisi Wasyria tutajikuta tukiona aibu maisha yetu yote." Amesema Assad.

Assad alisema kiwango cha damu kinachomwagwa nchini mwake ni cha kufadhaisha kwa sababu ni damu ya Wasyria inayomwagwa kwa maslahi ya wageni, akisema ni afadhali kama angalau damu hiyo ingelimwagwa kwa ajili ya kuikomboa milima ya Goland kutoka mikononi mwa Israel.

Hotuba hiyo ya jana bungeni, ambayo ilirushwa moja kwa moja na televisheni ya taifa ilichukuliwa kama majibu kwa shinikizo la kimataifa dhidi yake, hasa baada ya mauaji ya Hawla, ambayo Rais Assad alisisitiza kwamba yalifanywa na magaidi wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni na sio jeshi lake wala wanamageuzi wa kweli wanaotaka mageuzi ya kisiasa.

Marekani yaishinikiza Urusi kuchukuwa hatua

Kwa upande mwengine, Marekani imetumia fursa ya mauaji ya Houla kuongeza mbinyo wake dhidi ya Syria na washirika wake. Akizungumza mjini Stockholm, Sweden, baada ya kumaliza ziara yake ya mataifa ya Scandinavia hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, aliitaka Urusi kuungana na jumuiya ya kimataifa kumaliza umwagikaji damu nchini Syria. Clinton amesema amezungumza na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov, na kumtaka aisaidie Syria kubadilika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton.Picha: dapd

"Niliweka wazi kwamba hakutakuwa na haja ya kukutana isipokuwa mkutano huo ujumuishe masuala ya mpango wa amani wa Annan, na kwamba kuwe na njia maalum tunazopaswa kuziangalia kwa ajili ya kipindi cha mpito cha kisiasa nchini Syria. Kuondoka kwa Assad madarakani hakupaswi kuwa sharti, bali matokeo." Amesema Clinton.

Urusi na China zimekuwa zikichukuliwa kama mataifa yanayompa kinga Rais Assad kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na zimekuwa zikilaumiwa kuachia damu kumwagika nchini Syria bila ya kuchukuwa hatua muafaka. Hivi leo, Rais Vladimir Putin anakutana na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya mjini Saint Petersburg, ambapo wakuu hao wanatarajiwa kumshawishi kubadili msimamo wake kuelekea Syria.

Annan ataka uhakiki mpya wa mpango wake

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Urusi iliyotolewa jana, imesema kwamba nchi hiyo inasubiri matokeo ya uchunguzi juu ya mauaji ya Hawla na kwamba imekerwa na baadhi ya nchi ambazo tayari zimeshafikia umbali wa kuchukua hatua na kuilaani serikali ya Syria.

Mjumbe wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan.
Mjumbe wa kimataifa kwa Syria, Kofi Annan.Picha: picture-alliance/dpa

Wakati hayo yakiendelea, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa Syria, Kofi Annan, ametaka kuwepo kwa uhakiki wa hali ya juu wa jitihada zilizokwama za kumaliza ghasia na umwagaji damu, jambo linalotafsiriwa na wengi kwamba hata naye sasa ameanza kukosa stahmala.

Wanadiplomasia wanasema Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa, ameongeza shinikizo kwa mataifa makubwa duniani kuongeza nguvu zao katika mpango wake wa amani au kutafuta kile kinachoitwa Plan B. Annan amesisitiza kwamba wakati wa kuupitia upya mpango wake umewadia, akisema kwamba jumuiya ya kimataifa lazima iamue sasa kile kitakachofuata baadaye.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf