1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad ayataka majeshi ya Marekani kuondoka Syria

Caro Robi
31 Mei 2018

Rais wa Syria Bashar al Assad amesema Marekani inapaswa kujifunza kutokana na  mzozo wa Iraq na kuyaondoa majeshi yake kutoka Syria, akiahidi kuyakomboa maeneo yote yanayodhibitiwa na waasi kupitia mazungumzo au nguvu. 

https://p.dw.com/p/2yhSj
Syrien Bashar Assad im Interview in Damaskus
Picha: picture-alliance/AP Photo/SANA

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Russia Today, Assad amesema serikali yake imeanza kufungua milango kwa ajili ya mazungumzo na kikosi cha wapiganaji cha Syrian Democratic Forces, SDF, kundi la waasi wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani linalodhibiti maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Syria ambako majeshi ya Marekani yamekita kambi. SDF inasemekana kudhibiti thuluthi moja ya Syria.

Rais huyo wa Syria amesema mazungumzo ndiyo njia ya kwanza watakayotumia, kuafikiana na kundi hilo la Kikurdi la SDF na iwapo hilo litashindikana, basi watalazimika kuyakomboa maeneo yanayodhibitiwa na SDF kwa kutumia nguvu kwani hawana budi kufanya hivyo iwe kupitia ushirikiano na Marekani au la, akiwataka Wamarekani kuondoka nchini Syria.

Assad aitaka Marekani kukumbuka iliyojifunza Iraq

Assad ametolea mfano wa Iraq, akisema Majeshi ya Marekani yaliivamia na kuingia nchini humo bila ya kuwa na msingi wowote kisheria na sasa nchi hiyo imesalia kuwa katika mzozo. Rais huyo wa Syria amesema watu hawatakubali wageni kuziingilia nchi za kanda hiyo ya Mashariki ya Kati tena.

Syrien Abu Omar al-Idlibi von der SDF in ar-Raqqa
Kiongozi wa SDF Abu Omar al Idlibi(Aliyesimama Katikati)Picha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Alipoulizwa na kituo hicho cha televisheni cha Russia Today kuhusu mtizamo wa Rais wa Marekani Donald Trump kuwa yeye ni myama, Assad amesema kile unachokisema kumhusu mtu mwingine ndivyo ulivyo. Trump alimuita Assad mnyama baada ya shambulizi linalodaiwa kuwa la silaha za sumu katika eneo Douma mnamo mwezi Aprili.

Serikali ya Syria kwa mara nyingine imekanusha kuwa ilitumia silaha za sumu dhidi ya raia wake ikisisitiza haina silaha hizo za sumu wala haikuwa na nia yoyote ya kufanya shambulizi la aina hiyo. Marekani, Uingereza na Ufaransa ziliishambulia Syria kwa makombora baada ya shambulizi hilo la Douma zikisema zinalenga maeneo ya kijeshi ambako silaha za sumu zinahifadhiwa.

Assad amefanikiwa kuyadhibiti maeno mengi nchini humo yaliyokuwa mikononi mwa waasi kufuatia jeshi lake kuungwa mkono na Urusi na Iran, Mzozo wa Syria ulioanza mwaka 2011 umesababisha vifo vya maelfu kwa maelfu ya watu na kuwaacha mamilioni ya wengine bila ya makazi au wakimbizi.

SDF na majeshi ya serikali ya Syria yanayoungwa mkono na Urusi yamekuwa yakifanya opresheni tofauti za kijeshi dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS mashariki mwa Syria na hivyo kulifanya eneo hilo kushuhudia mapambano makali.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri:Yusuf Saumu