1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad:Tunakaribisha mapendekezo ya kijeshi ya Urusi

Hawa Bihoga
16 Machi 2023

Rais wa Syria Bashar Al-Assad amesema anakaribisha mapendekezo yoyote ya Urusi ya kuweka kambi mpya za kijeshi za kudumu na kuongeza idadi ya wanajeshi katika taifa hilo la Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4OlCX
Russland, Moskau | Syriens Präsident Assad in Russland
Picha: SANA/dpa/picture alliance

Akiwa ziarani mjini Moscow tangu jana Jumatano, Assad aliunga mkono kile Ikulu ya Urusi, Kremlin inakiita oparesheni ya kijeshi nchini Ukraine na kuliambia shirika la habari la Urusi kwamba Damascus inatambua maeneo ambayo yanadaiwa na Urusi nchini Ukraine.

Katika mahojiano yake alioyafanya leo Alhamisi Assad amesema Syria inakaribisha mapendekezo yoyote ya Urusi kuanzisha kambi mpya na za kudumu za kijeshi na kuongeza idadi ya askari wa Urusi.

Assad ameongeza kuliambia shirika la habari la Urusi RIA kwamba ikiwa Urusi inawiwa kutanua kambi ni suala la kiufundi ama vifaa.

Hapo jana Assad akilakiwa na kuingia katika mazungumzo na mwenyeji wake Rais Vladmir Putin, alimuhakikishia kwamba ingawaje taifa hilo lipo kwenye hali ya vita, lakini misimamo yake ni ile ile na haijawahi kubadilika.

Soma pia:Rais Vladmir Putin amempokea rais wa Syria Bashar al-Assad

Akisisitiza msimamo wa Syria Assad amesema taifa lake linaunga mkono vita hivi dhidi ya unazi wa zamani na mambo leo.

"Nasema unazi huu wa zamani na mambo leo sababu uliungwa mkono na Magharibi kabla ya Vita vya Pilivya Dunia, ilikumbatia viongozi wake baada ya vita, na inaendelea kuwaunga mkono kama hapo awali."

Wizara za ulinzi Urusi,Syria zaingia kwenye majadiliano

Hapo jana Jumatano waziri wa ulinzi Urusi Sergei Shoigu alikutana na mwenzake wa Syria Mahmoud Abbas mjini Moscow na kujadili kuhusu hali ya Syria na ushirikiano wa kijeshi wa pande mbili.

Russland Verteidigungsminister Sergej Schoigu verkündet Umbau der Armee
Wakuu wa kijeshi wakiwa katika mkutano wakiongozwa na waziri wa ulinzi Urusi Sergei Shoigu Picha: Russian Defence Ministry/AP/picture alliance

Majadiliano hayo yalitarajiwa pia kulenga kuijenga upya Syria baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoharibu na kurekebisha uhusiano wa Damascus na Ankara.

Shoigu alimwambia Abbas kwamba tayari mataifa hayo mawili yamepata mafanikio makubwa katika kuikomboa Syria katika changamopto chungumzima ikiwemo ugaidi.

"Bila shaka kuna kazi kubwa mbele yetu ,lakini wakati huo huo kazi kubwa tumefanya."

Urusi iliingilia kijeshi vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria mnamo 2015 ikiwa ni msaada mkubwa kwa upande wa Assad na kumhakikishia kiongozi huyo wa Syria anasalia madarakani, licha ya mataifa ya Magharibi kudai aondolewe.

Soma pia:Je Bashar al Assad anarejea hatua kwa hatua kwenye ulingo wa diplomasia ya kimataifa?

Kando ya kambi ya anga ya Hmeimim, ambapo Urusi ilizindua mashambulizi ya anga kumuunga mkono Assad, Moscow pia inadhibiti kituo cha wanamaji cha Tartus nchini Syria, kituo chake pekee cha jeshi la majini katika Bahari ya Mediterania, inayotumika tangu siku za Umoja wa Kisovieti.

Wizara ya ulinzi ya Russia ilisema mwezi Januari kwamba Urusi na Syria zimerejesha kambi ya kijeshi ya al-Jarrah iliyoko kaskazini mwa Syria ili kutumika kwa pamoja. Kambi hiyo ndogo mashariki mwa Aleppo ilitekwa tena kutoka kwa wapiganaji wa dola la Kiislam mnamo 2017.