AU Kampala
24 Julai 2010KAMPALA:
Jeshi la Umoja wa Afrika linalopambana na waasi wa Somalia wanaohusiana na Alkaida litaimarishwa kwa vikosi kutoka Guinea na kufikia idadi ya askari alfu 10.
Taarifa hiyo imetolewa kwenye kikao cha mawaziri wa nchi za Umoja wa Afrika wanaokutana mjini Kampala kabla ya kikao cha kilele cha viongozi wa Umoja huo.
Kwa sasa Umoja wa Afrika una askari kutoka Uganda na Burundi waliopo nchini Somalia.
Na Rais wa tume ya Umoja wa Afrika Jean Ping amewaambia wandishi habari mjini Kampala kwamba Djibouti nayo ipo tayari kuchangia majeshi.
Kuhusu Guinea bwana Ping amesema nchi hiyo inataka sana kupeleka majeshi nchini Somalia.
Mkutano wa nchi za Umoja wa Afrika unafanyika katika mji mkuu wa Uganda Kampala wiki mbili tu baada ya magaidi kufanya mashambulio katika mji huo na kuwaua watu 76 waliokuwa wanatazama fainali ya kombe la dunia.
Al Shabaab,kundi linalohusiana na Alkaida lilisema kuwa lilifanya shambulio hilo.