1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yakutana na wawakilishi wa Niger, ECOWAS

14 Agosti 2023

Umoja wa Afrika ulikutana na wawakilishi wa Niger na Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kuzungumzia mzozo wa kisiasa nchini Niger, huku jeshi likisema lingelimfungulia Rais Mohamed Bazoum kesi ya uhaini.

https://p.dw.com/p/4V99t
Kenia Moussa Faki Mahamat AU
Picha: Simon Maina/AFP

Kupitia mtandao wa X, Umoja wa Afrika ulisema siku ya Jumatatu (Agosti 14) kwamba Baraza la Amani na Usalama lilikuwa linakutana kupokea taarifa juu ya mwenendo wa mambo nchini Niger na juhudi kuitatuwa hali ya mambo. 

Mkutano huo ulifanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, ilisema taarifa hiyo. 

Soma zaidi: Waziri wa Ujerumani ametowa mwito kutafutwa njia amani Niger

Kikao hicho cha dharura kilihudhuriwa na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, na wawakilishi kutoka Niger na Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

Kesi ya uhaini dhidi ya Bazoum

Wiki iliyopita, Faki alielezea wasiwasi wake juu ya hali mbaya aliyonayo Bazoum akiwa kizuizini, akisema kuwa jinsi anavyotendewa na viongozi wa mapinduzi ya kijeshi lilikuwa "jambo lisilokubalika."

Nigers Präsident Mohamed Bazoum | Archivbild
Hali ya Rais Mohamed Bazoum aliye mikononi mwa jeshi la nchi yake inatajwa kuzidi kuwa mbaya.Picha: Evelyn Hockstein/Pool/File Photo/REUTERS

Siku ya Jumapili (Agosti 13), utawala huo wa kijeshi ulisema unakusudia kumfungulia kiongozi huyo aliyechaguliwa kidemokrasia kesi ya uhaini wa kiwango cha juu, huku wakilaani vikwazo vilivyowekwa na ECOWAS ambayo tayari imeshatangaza uwezekano wa kuchukuwa hatua za kijeshi.

Soma zaidi: Utawala wa kijeshi kumfungulia mashtaka ya uhaini Bazoum

Rais Bazoum, mwenye umri wa miaka 63, na familia yake wamekuwa wakishikiliwa kwenye makaazi rasmi ya rais mjini Niamey tangu alipopinduliwa.

Niger yaapa kupambana na vikwazo 

Hayo yakijiri, waziri mkuu mpya wa utawala wa kijeshi wa Niger, Ali Mahaman Lamine Zeine, amesema nchi yake itaweza kukabiliana na vikwazo vya ECOWAS, ambavyo si halali na itashinda.

"Maisha ya mwanadamu yameundwa na changamoto, na tunaona kwamba hata ikiwa ni changamoto isiyo ya haki kwetu, tunapaswa kushirikiana ili kuishinda. Na tutashinda.  Hakuna hofu katika suala hili. Wananchi wa Niger wamedhamiria kufanya hivyo na ninaamini kwamba chini ya uongozi wa Mkuu wa Nchi na timu nzima inayomzunguka, kwa msaada wa watu wetu wote, lakini juu ya yote, kwa msaada wa Mungu, mambo yatakwenda vizuri." Alisema kwenye mahojiano yake na DW yaliyochapishwa siku ya Jumatatu (Agosti 14).

Niger Interview Ali Mahaman Lamine Zeine
Waziri Mkuu mpya wa Niger, Ali Mahaman Lamine Zeine, anaamini kuwa nchi yake itaweza kuvishinda vikwazo ilivyowekewa na jumuiya ya ECOWASPicha: DW

Soma zaidi: ECOWAS na juhudi za kidiplomasia kwenye mzozo wa Niger

ECOWAS imeiwekea Niger vikwazo vya kifedha, imeikatia umeme na kuifungia mipaka yake yote na, kwa kufanya hivyo, imezuwia bidhaa zozote kuingia kwenye taifa hilo masikini kabisa lisilokuwa na bahari.

Utawala wa kijeshi umesema hatua hiyo imeongeza ugumu kwa watu kupata madawa, chakula na umeme na kuvielezea kuwa vikwazo hivyo kuwa "haramu, visivyo vya kibinaadamu na vya udhalilishaji."

Vyanzo: DW, Reuters, AFP