AU yapongeza makubaliano ya nafaka kati ya Urusi na Ukraine
23 Julai 2022Mashamba ya Ukraine ni chanzo kikuu cha nafaka katika soko la dunia, hasa katika maeneo ya Mashariki ya Kati na Afrika, ambapo usambazaji wa chakula umekuwa ni mdogo sana tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Shirika hilo limesema makubaliano hayo ni matokeo ya ziara ya mwezi Juni nchini Urusi ya Mwenyekiti wa tume ya AU na rais wa Senegal Macky Sall, ambaye alisisitiza kwa Rais Vladimir Putin, dharura ya kupelekwa nafaka kutoka Ukraine na Urusi katika masoko ya dunia.
Rais Sall pia amemshukuru Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye alisimamia hafla ya utiaji saini mjini Istanbul mnamo siku ya Ijumaa, pamoja na marais wa urusi Vladimir Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr kwa kufikia makubaliano hayo muhimu.
Umoja wa Afrika pia umetoa wito wa kusitisha mara moja mapigano nchini Ukraine na kuanzishwa kwa mazungumzo mapya ya kisiasa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa kwa maslahi ya amani na utulivu duniani.
Bei ya nafaka katika bara la Afrika imepanda kwa sababu ya kudorora kwa mauzo kutoka nje, na hivyo imeongeza athari za migogoro na mabadiliko ya hali ya hewa hali inayosababisha hofu ya kutokea machafuko miongoni mwa kijamii.
Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji IRC inayoshughulika na kuwasaidia watu walioathiriwa na majanga, pia imesema imefurahishwa na makubaliano hayo,na kuongeza kwamba nchi za Afrika Mashariki zinazitegemea Urusi na Ukraine kwa zaidi ya asilimia 90 ya ngano inazoagizwa kutoka nje.
Mkurugenzi wa halia ya dharura wa shirika hilo la kimataifa la IRC kanfa ya Afrika Mashariki, Shashwat Saraf amesema kuondolewa kwa vizuizi hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza njaa kali kwa zaidi ya watu milioni 18 katika nchi za Afrika Mashariki na wengine milioni tatu ambao tayari wanakabiliwa na hali mbaya ya baa la njaa.
Wanadiplomasia wanatarajia shehena za nafaka kuanza kusafirishwa kikamilifu kuanzia katikati ya mwezi Agosti kwa sababu pande zote lazima kwanza zianzishe kituo cha pamoja cha usimamizi mjini Istanbul, Uturuki ambacho kitafuatilia safari za meli za nafaka na jinsi meli hizo zitakavyokaguliwa ili kubaini iwapo hazikubeba silaha kabla ya kuruhusiwa kurejea kwenye bandari za Ukraine.
Wakati huo huo serikali ya Ukraine imelaani kitendo cha Urusi cha kuishambulia bandari ya Odessa iliyo katika Bahari Nyeusi, sikunmmoja tu baada ya makubaliano kufikiwa na imesema imesema kwamba hiyo ni ishara ya kuudharau Umoja wa Mataifa pamoja na Uturuki zilizosimamia majadiliano na hatimaye kufikia makubaliano ya kuruhusu tena usafirishaji wa nafaka nje.
Ukraine imeitupia lawama Urusi na kusema kwamba itawajibika kwa mgogoro wowote wa chakula iwapo makubaliano hayo yatavunjika. Balozi wa Marekani nchini Ukraine Bridget Brink amesema Moscow inapaswa kuwajibishwa kwa alichokiita "mashambulizi ya kutisha" kwenye mji wa bandari wa Odesa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa antonio Guterres amelaani vikali mashambulio hayo katika bandari ya Odesa nchini Ukraine. Amkumbusha kwamba pande zote zimetoa ahadi ya kuhakikisha harakati salama za kusafirishwa nafaka na kupelekwa kwenye masoko ya kimataifa. Amesema bidhaa hizi ni ziinahitajika sana ili kupunguza mgogoro wa chakula duniani na kuwaondolea mateso mamilioni ya watu wanaohitaji msaada kote ulimwenguni.
Vyanzo:AFP/RTRE