Aubameyang aizamisha Hamburg SV
7 Novemba 2016Matokeo katika uwanja wa Allianz Arena yana maana RB Leipzig ambayo iko katika nafasi ya pili inaweza kufikisha pointi sawa na mabingwa hao watetezi, pointi 24 juu ya kilele cha Bundesliga iwapo watashinda nyumbani kwa timu iliyoko katika nafasi ya kati ya Mainz 05 leo Jumapili,(06.11.2016).
Yalikuwa matokeo mazuri kwa Hoffenheim, ambayo inaendeleza mwendo wa kutofungwa hadi sasa msimu huu chini ya kocha mwenye umri wa miaka 29 Julian Nagelsmann.
Lakini siku ya jana Jumamosi ilikuwa ya Aubameyang , ambaye alijirudi kutokana na matatizo aliyojiletea katikati ya wiki kwa kufunga mabao safi wakati Dortmund iliposhinda kwa mara ya kwanza katika michezo mitano ya ligi na kuchupa hadi nafasi ya tano.
Aubameyang alisimamishwa kwa muda na kocha Thomas Tuchel katika mchezo wa Jumatano ambao Dortmund ilishinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa Champions League nyumbani dhidi ya Sporting Lisbon baada ya kwenda Milan kwa ndege ya binafsi pamoja na marafiki siku ya Jumatatu.
Lakini kila kitu kilionekana kupata msahama mjini Hamburg wakati mshambuliaji huyo raia wa Gabon aliposherehekea bao lake la kwanza kwa kumwendea kocha Tuchel na kumkumbatia kwa vicheko.
Aubameyang acharuka
"Auba" alihitaji dakika 27 tu kupachika mabao matatu ya kwanza na kufunga bao la nne katika kipindi cha pili. "nilifanya makosa na ilibidi kuomba msamaha. Nilishasema "samahani" kwa timu na kocha," Aubameyanga alikiambia kituo cha televisheni cha Sky.
"Nilihitaji kutoa huduma yangu kwa timu nzima na kocha, ambae tunaelewana sana." Alifunga bao la kwanza la Dortmund dakika nne tu tangu kuanza mchezo.
Huu ulikuwa mchezo mbovu kabisa kwa Hamburg na sio kile ambacho mchezaji mkongwe wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani Uwe Seeler alivyopondelea katika siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 80 , wakati akishuhudia klabu yake ikikubali kipigo cha nane katika michezo 10 ya Bundesliga.
Mjini Munich , Bayern walinyimwa ushindi mara ya sita mfululizo na timu iliyoko katika nafasi ya tatu ya Hoffenheim , ambayo iliendeleza rekodi yake ya kutofungwa msimu huu.
Kerem Demirbay alipachika bao baada ya kupata pasi safi kutoka kwa Nadiem Amiri katika dakika ya 16, lakini bao hilo halikudumu muda mrefu.
Mchezaji wa kati wa Hoffenheim Steven Zuber alijifunga mwenyewe katika dakika 34 wakati Robert Lewandowski akisubiri katika nguzo ya goli.
Baada ya kuishinda Tottenham Hotspur ugenini katika Champions League katikati ya wiki , Bayer Leverkusen ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Darmstadt kwa magoli ya Hakan Calhanoglu, Julian Brandt na Charles Aranguiz.
Wolfsburg yazinduka
Wolfsburg ilijitoa kutoka katika eneo la kushuka daraja hadi nafasi ya 13 baada ya ushindi wa mabao 3-0 huku kukinyesha mvua kubwa dhidi ya wachezaji 10 wa Freiburg wakati mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani Mario Gomez alifunga mara mbili wakati Ricardo Rodriguez alipachika bao kwa mkwaju wa penalti. wakati huo huo kocha wa mpito Valerien Islamael atabakia kuwa kocha mkuu wa VFL Wolfsburg kwa wakati huu, klabu hiyo ya Bundesliga imesema leo Jumapili baada ya ushindi hapo jana Jumamosi wa mabao 3-0 dhidi ya Freiburg.
Magoli ya dakika za mwisho kutoka kwa mchezaji aliyetokea kutoka benchi akiwa mchezaji wa akiba Raul Bobadilla na Halil Altintop yaliipata Augsburg ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ingolstadt.Na kocha wa timu hiyo ya Ingolstadt Markus Kauczinski amefutwa kazi na klabu hiyo leo Jumapili baada ya kipigo hicho, timu hiyo ikiwa na mwanzo mbaya kabisa katika ligi ya Bundesliga msimu huu, ikiwa na pointi 2 na haijawahi kushinda hadi katika mchezo wa 10.
Mchezo wa mwisho jana Jumamosi ulikuwa kati ya FC Cologne na Eintracht Frankfurt. FC Cologne iliporomoka hadi nafasi ya sita baada ya kukandikwa bao 1-0 na Eintracht Frankfurt, bao pekee ilililofungwa na mchezaji wa kati Mijat Gacinovic dakika tano baada ya mchezo huo kuanza.
Siku ya Ijumaa Hertha Berlin iliiogesha Borussia Moenchengladbach bila sabuni kwa kuizaba mabao 3-0, wakati Salom Kalou alipopachika mabao yote matatu ikiwa ni mabao yake ya kwanza tangu mwezi Aprili mwaka huu.
Anthony Modeste pamoja na Pierre Emerick Aubameyang wanaongoza ufungaji mabao katika Bundesliga , ambapo kila mmoja amepachika mabao 11. obert Lewandowski wa Bayern Munich anafuatia akiwa na mabao 7. Vedad Ibisevic ana mabao 6 na Yunus Mali wa Mainz ana mabao 5.
Loew ateua chipukizi katika Die Mannschaft
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew ametaja kikosi chake na kuwaita wachezaji watatu wapya katika kikosi hicho kwa ajili ya pambano la kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi dhidi ya San marino na mchezo wa kirafiki dhidi ya Italia.
Kijana chipukizi wa Bayer Leverkusen Benjamin Henrichs, Yannick Gerhardt mwenye umri wa miaka 22 kutoka VFL Wolfsburg na Serge Gnabry aliyepata medali ya fedha akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani katika michezo ya Olimpiki , ambaye anaonesha mchezo safi akiwa na kikosi cha Werder Bremen wote wamejumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa.
Ujerumani inasafiri kwenda San Marino katika pambano la kufuzu fainali za kombe la dunia Novemba 11 kabla ya kupambana na Italia katika mchezo wa kirafiki mjini Milan siku nne baadaye.
Grindel rais wa DFB
Reinhard Grindel alichaguliwa tena siku ya Ijumaa kuwa rais wa shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB kwa kipindi kamili cha miaka mitatu baa ya kuchukua nafasi ya Wolfgang Niersbach , ambaye alijuzulu mwaka jana kwa kuhusika na masuala ya kombe la dunia mwezi Aprili.
Grindel alipata kura zote kutoka kwa wajumbe 258 katika mkutano wa DFB mjini Erfurt.
Grindel mwenye umri wa miaka 55 ana lengo la kuliweka katika hali ya kisasa zaidi shirikisho hilo la DFB ambalo ndio shirikisho kubwa kabisa la taifa katika mchezo mmoja duniani likiwa na wanachama zaidi ya milioni 6.
Mageuzi yanahitajika kutokana na suala linalozunguka kombe la dunia mwaka 2006, ambapo Ujerumani ilikuwa mwenyeji , hali inayoweka kiwingu katika soka la Ujerumani.
Chelsea kidedea
Kocha wa Chelsea ya Uingereza Antonio Conte amedai kwamba timu yake inaweza kuwa bora zaidi, licha ya kupata ushindi wake mzuri zaidi akiwa kocha wa timu hiyo hadi sasa, akiueleza ushindi wa kikosi chake wa mabao 5-0 dhidi ya Everton kuwa ni mzuri sana.
Pep Guardiola alikiri Manchester City inahitaji kujenga uwezo mkubwa wa kufunga mabao baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Middlesbrough. Kikosi cha Guardiola kilipiga hatua kubwa katika medani ya ulaya wakati walipoirarua barcelona kwa mabao 3-1 katika Champions League siku ya Jumanne.
Lakini siku nne baadaye City wanaonekana kuwa wachovu baada ya kipindi cha kwanza ambapo walicheza vizuri.
Mabingwa wa Afrika hoi
Mabingwa wapya wa Afrika Mamelodi Sundowns wameondolewa katika kombe la ligi la Afrika kusini jana jumamosi baada ya kupoteza mchezo wa robo fainali kwa njia ya penalti dhidi ya watu 10 uwanjani wa kikosi cha Super Sport United.
Pambano hilo la watani wa jadi mjini Pretoria liliishia kwa sare ya bila kufungana baada ya dakika za nyongeza katika uwanja wa Lucas "Masterpieces" Moripe na SuperSport waliwaangusha mabingwa hao watetezi kwa mikwaju 3-1.
Gebreselassie rais wa riadha Ethiopia
Mkimbiaji wa mbio ndefe Haile Gebreselassie alichaguliwa kuwa rais wa shirikisho la wanariadha nchini Ethiopia siku ya Jumamosi baada ya kusema mchezo huo nchini mwake "umeingia doa" kwa madai ya matumizi ya dawa zinazoongeza nguvu misuli na alitaka , "kusafisha hali hiyo".
Bingwa mara mbili wa Olimpiki katika mbio za mita 10,000 alipata kura 15 katika uchaguzi uliowahusisha viongozi wa majimbo wa vyama vya riadha.
Aliwashinda wagombea wengine wawili , ikiwa ni pamoja na rais aliyekuwa madarakani Alebachew Nigusse ambaye hakugombea.
Haile Gebreselassie amechaguliwa kwa kipindi cha miaka minne.
Wakimbiaji wanaokadiriwa kufikia 50,000 , ikiwa ni pamoja na bingwa wa mwaka jana Mkenya , wamejiandikisha kushiriki katika mbio za marathon za mjini New York leo Jumapili(06.11.2016).
Mani Pacquiao
Manny Pacquiao alionesha kwamba bado anazo nguvu za kutosha kwa kumtwanga Jessie Vargas katika pambano la mkanda wa WBO siku ya Jumamosi, na hasimu wake Floyd mayweather alikuwapo kushuhudia pambano hilo akikaa karibu kabisa na ulingo wa pambano.
Pacquiao ambaye , ambaye anafikia umri wa miaka 38 mwezi ujao, alimuangusha chini Vargas katika duru ya pili wakati akielekea kushinda pambano hilo lililikuwa la upande mmoja ambapo ushindi huo unamruhusu kunyakua pia taji la WBO uzito wa Welter ambao yeye pamoja na Mayweather waliushikilia hapo kabla.
Ni taji pekee ambalo Pacquiao alilitema wakati aliposhindwa mwaka jana na Mayweather katika pambano lililoingiza fedha nyingi zaidi katika historia ya ngumi za kulipwa.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Dahman