Aubameyang ang'ara tuzo za Afrika.
8 Januari 2016Katika kura hiyo iliyohusisha makocha na wakurugenzi wa ufundi wa mataifa wananchama wa shirikisho la kandanda barani Afrika (CAF) Aubameyang alijikusanyia alama 143 na kumshinda Yaya Toure anaekipiga katika kilabu ya Manchester City ya Uingereza aliyepata alama 136 na ambaye alikuwa akiwania tuzo yake ya tano.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Ghana na kilabu ya Swansea ya Uingereza Andre Ayew alishika nafasi ya tatu akipata alama 112.
Ushindi huu wa Aubameyang unaonekana kumpa faraja baada ya kushindwa na Yaya Toure katika tuzo hizo mwaka 2014 ambaye pia aling'ara katika tuzo za mwaka 2011,2012 na 2013.
Nyota huyo wa Gabon mwenye umri wa miaka 26 kwa sasa ameonyesha pia kiwango kizuri msimu huu katika ligi ya kandanda ya Ujerumani Bundesliga akiichezea kilabu ya Borussia Dortmund ambapo pia tangu alipoanza kucheza katika ligi hiyo ya Ujerumani akitokea klabu ya Saint- Etienne mwaka 2013 amefanikiwa kupachika mabao 18 katika michezo 17 ya ligi hiyo ya kandanda ya Ujerumani.
Mafanikio hayo katika kipindi kifupi yamemfanya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Gabon kuwa kivutio kikubwa wakati wa usajili wa msimu wa baridi akiwindwa na vilabu vya Uingereza vya Arsenal, Liverpool pamoja na Manchester United.
Herve Renard kocha bora.
Mfaransa Herve Renard ambaye aliiongoza Cotte D'Voire katika fainali za mataifa ya Afrika za mwaka jana alitangazwa kuwa kocha bora wa mwaka barani Afrika ikiwa ni tuzo yake ya pili baada ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 47 kuiwezesha Zambia kutwaa ubingwa wa Afrika katika fainali za mwaka 2012.
Timu ya taifa ya Cotte D' Voire ilitangazwa kuwa timu bora ya mwaka ya Afrika.
Washindi wengine wa tuzo hiyo ni Gaell Enganamouit wa Cameroon aliyenyakua tuzo ya mchezaji bora wa Afrika kwa upande wa wanawake, kilabu ya TP Mazembe ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo ikinyakuwa tuzo ya kilabu bora barani Afrika wakati kiungo wa timu ya taifa ya vijana ya Nigeria ya chini ya umri wa miaka 23 Oghenekaro Etebo akitangazwa kuwa mchezaji bora mwenye kipaji anayechipukia .
Mchezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Nigeria chini ya umri wa miaka 17 Victor Osimhen alijinyakulia tuzo ya mchezaji bora kijana wa mwaka barani Afrika.
Rais Ali Bongo ampongeza Aubameyang
Rais wa Gabon Ali Bongo Ondimba alimpongeza Aubameyang kwa mafanikio hayo na kusema tuzo hiyo ya mchezaji bora wa Afrika itakuwa chachu na kuongeza morali kwa timu ya taifa ya Gabon kufanya vizuri katika fainali zijazo za mataifa ya Afrika za mwaka 2017 ambazo pia zimepangwa kufanyika nchini Gabon.
Wakati huo huo mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Tanzania anayechezea pia kilabu ya TP Mazembe ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbwana Samatta alitangazwa kuwa mchezaji bora barani Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani barani humo.
Kabla ya kujiunga na kilabu ya TP Mazembe nyota huyo alikuwa akiichezea kilabu maarufu nchini Tanzania ya simba alimaarufu wekundu wa msimbazi.
Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga