Aung San Suu Kyi ahukumiwa miezi 18 nyumbani
11 Agosti 2009Kiongozi wa upinzani nchini Burma au Myanmar,Aung San Suu Kyi,amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kazi ngumu kwa kuziendeya kinyume sheria za kifungo cha nyumbani,lakini mkuu wa utawala wa kijeshi Than Shwe ameibadilisha hukmu hiyo na kua kifungo cha miezi 18 cha nyumbani.Zaidi anasimulia Oummilkheir.
Korti maalum iliyofunguliwa katika jela ya Insein,kaskazini mwa mji mkuu Rangun,imemkuta na hatia bibi Suu Kyi ya kuvunja kanuni za tangu mwaka 2003 za kifungo chake cha nyumbani.
Analaumiwa kwa kumkaribisha kwa muda mfupi mmarekani John Yettow aliyeogolea hadi nyumbani kwake mwezi May mwaka huu.
Aung San Suu Kyi amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na kazi ngumu.Lakini waziri wa mambo ya ndani,jenerali Maung Oo,amesema,mkuu wa utawala wa kijeshi,Than Shwe ametia saini waraka maalum kubadilisha hukmu hiyo na kuigeuza kifungo cha nyumbani cha miezi 18.
Mshindi wa mwaka 1991 wa zawadi ya amani ya Nobel,bibi Suu Kyi,anaeongoza chama kikuu cha upinzani nchini Burma inayoitwa pia Myanmar-Jumuia ya taifa kwaajili ya demokrasia,amekua akinyimwa uhuru wake kwa kipindi cha miaka 14 kati ya 20 iliyopita.
"Ahsante kwa hukmu",amesema bibvi Aung San Suu Kyi kwa kejeli,baada ya adhabu kutangazwa.
Ikiwa hakuna msamaha utakaotolewa hadi mwaka 2010,bibi Aung San Suu Kyi hatoweza kutetea chaguzi zinazopangwa kuitishwa mwakani.
Jumuia ya kimataifa imepaza sauti kulaani hukmu hiyo.Umoja wa Ulaya umewataka watawala wa kijeshi wamuachie huru haraka na bila ya masharti kiongozi huyo wa upinzani na kutangaza wakati huo huo "hatua maalum" dhidi ya watalawa wa kijeshi.
Umoja wa Ulaya unapanga pia kuimarisha vikwazo,ikiwa ni pamoja na vya kiuchumi dhidi ya utawala wa kijeshi.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier anasema:
"Kutokana na hali namna iulivyo nchini Burma,sio tuu tutaitisha kikao cha baraza la usalama,bali pia tutazungumzia suala hilo katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi nane tajiri kiviwanda G8."
Waziri mkuu wa Uengereza Gordon Brown amesema "amehuzunishwa na kuhamakishwa" na hukmu dhidi ya mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel.
Nayo jumuia ya mataifa ya kusini mashariki ya Asia-ASEAN inapanga kuitisha mkutano wa dharura kuzungumzia hukmu dhidi ya kiongozi wa upinzani nchini Burma.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Malaysia Anifa Aman amesema kwa kuhukumiwa kifungo cha miezi 18 nyumbani Aung San Suu Kyi amefungiwa njia ya kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwakani,uchaguzi unaobidi kua huru na wa haki.
Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/afpf
Mhariri:M.Abdul-Rahman