Azerbaijan yatangaza vifo 10 vya raia wake
29 Septemba 2020Takibrani watu 95 wameuwawa katika mzozo huo ambao umeanza mwishoni mwa juma. Msemaji wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Steffen Seibert amesema kansela anataka pamoja na kusitishwa mapigano pande zote zirejee katika meza ya mazungumzo. Anasema kansela huyo wa Ujerumani amezungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Pashinyan hapo jana na leo hii Rais Ilham Aliyev.
Aidha ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ya upatanishi ya haraka ya kile ambacho kinaratibiwa na mataifa ya kundi la Minsk, lenye kuyajumuisha mataifa ya Ufaransa, Urusi na Marekani. Kauli kama hiyo awali ilitolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.
Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa na mapigano
Kupitia msemaji wake, Stéphane Dujarric, Guterres amesema ana wasiwasi mkubwa na mapigano mapya yaliozuka kufuatia mzozo wa eneo la Nargorno-Karabakh." Amelaani matumuzi ya nguvu na kusikitishwa na vifo vya watu. Katibu mkuu pia amesisitiza pande zote kusitisha mapigano, kuacha vurugu na kurejea katika mijadala yenye tija pasipo masharti au kuchelewa.
Miito iliyotolewa na viongozi hao imeanza kupokelewa kwa vitendo baada ya Ufaransa kusema itaitisha mkutano wenye kuhusisha kundi la mataifa yaliyomo kwenye mazungumzo ya amani ya Minsk. Pasipo kutaja muda, ofisi ya Rais Emmanuel Macron imesema itafanikisha jambo hilo katika siku chache zijazo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukutana kwa dharura
Wakati huo huo duru za kidipolomasia zinaeleza kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya mkutano wa ndani wa dharura wenye lengo la kujadili mgogoro huo wa eneo ambalo linakaliwa na jamii ya Waarmenia.
Ndani nchini Azerbaijan, Rais wa taifa hilo Ilham Aliyev leo amesema raia wa taifa lake 10 wamepoteza maisha tangu kuzuka kwa mapigano hayo Jumapili. Majeshi ya pande zote mbili, yaani Azerbaijan na Armenia yamekuwa yakitupiana lawama za kufyatuliana risasi katika eneo la mpakani na kwenye makazi ya watu.
Soma zaidi: Mapigano ya Armenia na Azerbaijan yauwa 59
Maeneo ya Yerevan na Baku, katika jimbo hilo la Nagorno-Karabakh yamekuwa na mgogoro wa kimipaka kwa miongo kadhaa, ambapo mapigano mengine kama haya, yaliyosababisha mauwaji yalitokea Julai 2016. Jimbo hilo lilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Azerbaijan baada ya vita vya miaka ya 90, ambavyo vinadaiwa kuyagharimu maisha ya watu takribani 30,000. Hakuna nchi hata moja ya dunia inayoutambua uhuru huo.
Mwandishi: Sudi Mnette/Vyanzo: RTR/AFPE/USUNTV