1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azimio la UN la muda wa kutoa misaada Syria lazua hisia

13 Julai 2022

Kumekuwa na hisia mseto kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada ya kiutu kufuatia hatua ya Umoja wa Mataifa kuongeza kwa miezi sita muda wa misaada kutolewa kwa watu wanaoihitaji nchini Syria.

https://p.dw.com/p/4E4lF
Syrien | Grenzübergang Bab al-Hawa
Lori la kusafirisha misaada ya kibinadamu likitokea Uturuki kuelekea Syria kupitia mpaka wa Bab al-HawaPicha: Omar Haj Kadour/AFP/Getty Images

Baada ya siku kadhaa za mkwamo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikubaliana jana kuongeza muda huo kwa miezi sita kama Urusi ilivyokuwa imetaka.

Hatua hiyo imepongezwa na naibu mshirikishi wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Mark Cutts ila shirika la misaada la Care, limevunjwa moyo na muda huo kuongezwa kwa miezi sita pekee.

Urusi mwishoni mwa wiki iliyopita ilitumia nguvu yake ya kura ya turufu kuzuia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililokuwa linaungwa mkono na mataifa ya Magharibi, la kuongeza muda huo kwa mwaka mmoja.

Soma pia: Mashambulizi ya Marekani Syria yadaiwa kuwajeruhi raia kadhaa

Jana Jumanne Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha azimio linalorefusha kwa miezi sita utaratibu wa usafirishaji wa misaada kupitia mpakani hadi nchini Syria.

Urusi ilidai muda huo huku wanachama wengine wakitaka urefushwe kwa mwaka mmoja. Hatua hiyo imepata uungaji mkono kutoka wanachama 12 kati ya 15 wa Baraza la Usalama, wakiwemo Urusi, China na kundi la baraza hilo la wanachama 10 wasio wa kudumu.

Mataifa ya Magharibi yalitaka kuongezwa muda wa mwaka mmoja yakihoji kuwa miezi sita haitoshi kupanga ipasavyo upelekaji wa misaada katika nchi ya Syria iliyoharibiwa kwa vita.

Uingereza, Ufaransa na Marekani zilijiepusha na kura hiyo. Utaratibu wa upelekaji wa msaada kwenye mpaka wa Uturuki na kuingia eneo linalodhibitiwa na waasi nchini Syria katika kivuko cha Bab al-Hawa ndio njia pekee ambayo msaada wa Umoja wa Mataifa unaweza kuwafikia raia bila kupitia maeneo yanayodhibitiwa na wanajeshi wa serikali.