Baada ya vipimo vya DNA: Watanzania wadai mafuvu ya watu wao
23 Septemba 2023Zablon Kiwelu hakujua kamwe kwamba fuvu la babu yake lilikuwa likifunikwa na vumbi katika chumba cha chini ya ardhi mjini Berlin ambako limetunzwa kwa miongo kadhaa. Ilikuwa katika warsha moja iliyofanyika karibu na Mlima Kilimanjaro mwanzoni mwa mwezi Septemba alipopata taarifa hizo kwa mara ya kwanza, kupitia nyaraka zilizotoka katika Wakfu wa Prussia kuhusu Urithi wa Kitamaduni (SPK).
Neno ''positive'' lilichapwa katika nyaraka hizo, kuthibitisha kwamba vipimo vya kitaalamu (DNA) vimethibitisha uhusiano wa kinasaba baina ya Kiwelu na mojawapo ya mafuvu yaliyopatikana katika Hospitali ya Charite ya mjini Berlin.
''Nilifurahi sana kwamba baada ya zaidi ya miaka 100, hatimaye tunajua mahali yalipokuwa mabaki ya babu yangu,'' alisema raia huyo wa Tanzania.
Alinyongwa na wanajeshi wakoloni kutoka Ujerumani
Fuvu husika limewekewa alama ya ''Akida'', jina walilopewa wapiganaji wa vyeo vya juu na washauri wa kiongozi wa kabila la Wachaga wakati huo.
Kwa mujibu wa Zablon Kiwelu, babu yake, Sindato Kiwelu alikuwa mshauri wa Chifu Mangi Meli, kiongozi wa Wachaga wa Kilimanjaro. Wanajeshi wa Kijerumani walimnyonga pamoja na watu wengine 18, wakiwemo maakida na machifu mnamo karne ya 19.
Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa baada ya kumnyonga Sindato Kiwelu, watawala wa ukoloni wa Kijerumani walimkata kichwa na kukipeleka mjini Berlin.
''Kwa wakoloni wa Kijerumani, mifupa, na hususan mafuvu, vilichukuliwa kama nyara za kivita, lakini pia vitu hivyo vilitumiwa katika utafiti wa kisayansi, aghalabu wenye malengo ya ubaguzi wa rangi,'' ameeleza Valence Silayo, mtaalamu wa akiolojia na vinasaba kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania.
Silayo aliongoza shughuli ya kuwatafuta nchini Tanzania, watu wenye uhusiano na mafuvu yaliyoko mjini Berlin, na pia aliandaa warsha ambamo matokeo ya utafiti wa vinasaba (DNA) yaliwasilishwa kwa familia husika.
Katika mradi mkubwa wa utafiti, wanasayansi kutoka Jumba la Makumbusho ya Historia ya Kale la Berlin, kwa ushirikiano na wenzao kutoka Rwanda, walichunguza asili ya mafuvu ya watu yapatayo 1,100 kutoka makoloni ya zamani ya Ujerumani katika eneo la mashariki mwa Afrika.
Rais wa Wakfu wa Prussia kuhusu Urithi wa Kitamaduni (SPK), Hermann Parzinger, aliiambia DW kuwa kupatikana kwa watu hai wenye uhusiano wa vinasaba na mafuvu matatu kupitia vipimo vya DNA ni ''muujiza'' mithili ya kupata sindano katika rundo la nyasi kavu.
Mbali na fuvu la Sindato Kiwelu, mafuvu mengine mawili mjini Berlin yaliunganishwa bila shaka yoyote na familia nyingine mbili nchini Tanzania, kwa kutumia vipimo vya sampuli za mate. Familia hizo ni kutoka ukoo wa Molelia ambao watu wao wanaishi katika wilaya ya Kibosho, na nyingine ni ukoo wa Chifu Mangi Sina, mtawala wa uliokuwa ufalme wenye nguvu pia katika wilaya hiyo hiyo ya Kibosho mkoani Kilimanjaro kaskazini mwa Tanzania.
Baada ya vita vya muda mrefu, jeshi la Mangi Sina liliwashinda wanajeshi wa Ujerumani (Schutztruppen) mwaka 1891, lakini Wajerumani walilipiza kisasi katika vita vingine mwaka 1893. Mara hii Mangi Sina alishindwa, ngome yake iliharibiwa, na wapiganaji wake walikamatwa. Chifu mwenyewe aliaga dunia miaka michache baadaye, mwaka 1897.
Lakini mwanawe na mrithi wa utawala, Molelia, alikuwa mpiganaji hodari aliyewashambulia Wajerumani kwa mara nyingine. Hata hivyo, naye alikamatwa.
''Siku ya tarehe 2 Machi, 1900 Chifu Molelia alinyongwa na Wajerumani, na kichwa chake kilipelekwa mjini Berlin kinakosalia hadi leo,'' ameeleza Valence Silayo.
Wanataka wafanyiwe mazishi ya kimila
Silayo amesema kuwa hali ya kwamba Wachaga hawakuweza kumzika kiongozi wao kulingana na mila zao ni jambo ambalo limekuwa na athari za muda mrefu.
''Hii ni kwa sababu Wachanga wanafuata kanuni kali kwamba jamaa zao ni lazima wazikwe mkoani Kilimanjaro na si kokote kwingine,'' alisema Silayo.
Mtaalamu huyo wa akiolojia alisema Wachaga wanaamini kuwa ikiwa mtu hatazikwa kwa utaratibu wa kimila, ''roho yake huendelea kuzunguka huku na huko hadi leo hii.''
''Tangu enzi hizo, Wachaga wanaamini kuwa majanga, matatizo ya kiuchumi, mavuno duni na matukio mengine mabaya vimetokana na roho hizo ambazo hazijapumzishwa kwa amani.''
Ni kwa ajili hiyo kwamba watu wa familia za wale ambao mafuvu yao yalipelekwa Ujerumani, wanataka mabaki yao yarejeshwe Tanzania haraka iwezekanavyo.
''Kwa Wajerumani hicho kinaweza kuonekana kama kitendo cha ishara tu,'' alisema Silayo, ''lakini kwa jamaa nchini Tanzania, zoezi hilo lina umuhimu mkubwa zaidi.''
Alisema hivi sasa Ujerumani ni mshirika muhimu wa Tanzania, na serikali mjini Berlin hudhamini miradi mingi ya maendeleo ya Tanzania, lakini ushirikiano huo haupaswi kuwa sababu ya kusahau historia ya ukoloni.
Silayo ameongeza kuwa ''Wajerumani wanapaswa kuwajibika, na kukiri kuwa waliyoyafanya yalikuwa kinyume cha haki za binadamu. Kwamba matendo yao hayakuwa ya haki, na kuomba radhi.''
''Kwa namna hiyo, misaada ya maendeleo itakuwa na maana zaidi.''
Chaguo gumu: Kuzikwa au kuwekwa katika makumbusho
Zablon Kiwelu anasema hajui hatma ya mabaki ya babu yake. Wazo la kupeleka fuvu lake katika makumbusho ni suala ambalo limefikiriwa.
Familia itaamua baada ya mabaki hayo kurejeshwa nchini Tanzania. Kulingana na utamaduni, mwili mzima unapaswa kuzikwa kulingana na mila.
''Lakini kwa sababu ni fuvu tu, sidhani kwamba litafanyiwa mazishi. Tutaliweka katika jumba la makumbusho, ambako watu kutoka duniani kote wanaweza kuja kuliona,'' alisema.
Tanzania imekuwa ikiiwekea shinikizo serikali ya Ujerumani, iwajibike kutokana na ukatili wa enzi za ukoloni Afrika Mashariki. Mwaka 2020, balozi wa Tanzania mjini Berlin Abdallah Possi alitoa rai kwa serikali ya Ujerumani kujadiliana juu ya fidia kwa uhalifu uliofanyika.
Zablon Kiwelu anasema atamwajiri mwanasheria atakayewasiliana moja kwa moja na serikali ya Ujerumani, na alisema kwa uhakika kuwa atakwenda Berlin mwaka huu kulichukua fuvu la babu yake na kulirejesha Tanzania.
Makala hii iliandikwa kwanza kwa Kijerumani, na imetafsiriwa na Daniel Gakuba
Mhariri: Mohammed Khelef