Harry Kane kutua Munich kwa vipimo vya afya
11 Agosti 2023Mshambuliaji wa timu ya taifa ya England Harry Kane amekubali kujiunga na Bayern Munich kwa ada ya rekodi ya Bundesliga kutoka Tottenham Hotspur na ripoti za ndani zinaeleza kuwa makubaliano yanaweza kufanywa rasmi leo.
Ripoti za Ujerumani na Uingereza zinasema kwamba nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 tayari yuko safarini kuelekea Munich kwa vipimo vya afya baada ya vilabu vyote viwili kuripotiwa kufikia makubaliano ya ada ya uhamisho ya Euro milioni 100 huku kukiwa na nyongeza ya Euro milioni 20.
Soma zaidi: Bayern kumnasa Kane hatimaye?
Kulikuwa na uvumi kwamba Kane angesalia Spurs licha ya makubaliano kati ya Bayern na Spurs lakini nahodha huyo wa timu ya taifa ya England alikuwa tayari ametoa kibali cha mwisho cha kujiunga na mabingwa hao wa Ujerumani
Gazeti la michezo la Bild la Ujerumani limeripoti kuwa uhamisho huo unaweza kuthibitishwa leo Ijumaa na kwamba anaweza kutambulishwa rasmi ndani ya Bayern Munich siku ya Jumamosi katika mchezo wa Super Cup kati ya Bayern Munich na RB Leizig.
Soma zaidi: Kane kujiunga na Bayern? Füllkrug kuhamia Leverkusen?
Harry Kane alikuwa amebakisha mwaka mmoja pekee kuitumikia Spurs na mmiliki wa klabu hiyo ya London Joe Lewis aliamua kumuuza badala ya baadaye aondoke bure pindi mkataba wake utakapokamilika mwakani.
Kane alipitia chuo cha mafunzo cha soka cha Spurs na ndiye mfungaji bora wa muda wote wa timu hiyo akiwa na mabao 280 katika mechi 435.
Anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu ya Premia akiwa amefunga mabao 213 tangu alipocheza kwa mara ya kwanza mwaka 2012, nyuma ya gwiji Alan Shearer mwenye mabao 260.
Harry Kane pia ameweka rekodi ya mfungaji bora wa timu ya taifa ya England akiwa na mabao 58.
Kuwasili kwake Ujerumani kunachukuliwa kama heshima kwa ligi kuu ya Bundesliga na hata zaidi kwa Bayern Munich, ambao wanatumai ataziba pengo la ushambuliaji lililowachwa wazi na Robert Lewandowski aliyejiunga na Barcelona miezi 12 iliyopita.