Baba Mtakatifu kukamilisha ziara yake Cuba
28 Machi 2012Ibada itakayoongozwa leo na Baba Mtakatifu katika uwanja wa mapinduzi ulioko Havanna, mji mkuu wa Cuba, itahudhuriwa na mamia kwa maelfu ya watu. Kiongozi wa zamani wa Cuba, Fidel Castro, ambaye sasa ana umri wa miaka 85, aliutumia uwanja huo alipokuwa madarakani kuzungumza na idadi kubwa ya watu na kutoa hotuba zilizochukua masaa mengi. Majengo yanayouzunguka uwanja huo wa kihistoria yamepambwa kwa mabango yanayoonyesha picha za viongozi wa mapinduzi Ernesto Guevara, aliyefahamika zaidi kwa jina la Che, na Camilo Cienfuegos.
Inatarajiwa kwamba Papa Benedict wa 16 ataendelea kutoa wito wa kufanyika mabadiliko nchini Cuba. Hilo ni jambo ambalo amekuwa akilisisitizia tangu kuwasili kwake nchini humo. Papa amezungumzia pia haja ya kufanyika mapatano na ameitaka Cuba kujenga jamii iliyo wazi zaidi. Makamu wa rais wa bunge la Cuba, Marino Murillo, alieleza kwamba Cuba haiko tayari kufanya mabadiliko. "Hapatakuwa na madiliko ya kisiasa nchini Cuba," alisema Murillo. "Tunataka kubadili mfumo wa kiuchumi na kuuimaraisha mfumo wa kijamaa. Hii ni kwa manufaa ya taifa letu."
Fidel Castro afurahi kukutana na Papa
Katika mazungumzo yake na rais wa Cuba, Raúl Castro, ambaye ni mdogo wake Fidel Castro, Baba Mtakatifu ameutaka uongozi wa Cuba ulipe kanisa nafasi kubwa zaidi na ameiomba serikali iifanye siku ya ijumaa kuu, ambapo wakristo hukumbuka kufa kwa Yesu Kristo, kuwa sikukuu ya kitaifa. Itakumbukwa kwamba Fidel Castro aliifanya sikukuu ya Krismasi itambulike tena kama sikukuu ya kitaifa baada ya mazungumzo na Papa John Paul wa pili, aliyeitembelea Cuba mwaka 1998.
Fidel Castro, jana alitangaza katika mtandao wa internet kwamba atakutana kwa muda mfupi na Benedict wa 16. Castro alieleza kwamba atafurahi kuonana na kiongozi huyo wa kanisa katoliki kama alivyofurahi alipokutana na Papa John Paul wa Pili.
Lawama zimetolewa kwa sababu Papa Benedict wa 16 hajapanga kukutana na upande wa upinzani nchini Cuba. Palikuwa na uvumi kwamba Papa angekutana na rais wa Venezuela, Hugo Chavez, ambaye yuko Cuba kwa ajili ya kupata matibabu ya saratani, lakini Chavez amasema kwamba hatoingilia ratiba ya Baba Mtakatifu.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/RTRE/AFPE
Mhariri: Mohammed-Abdul-Rahman