1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Wanajeshi wa Bahrain wafa katika shambulizi la waasi

26 Septemba 2023

Afisa mmoja pamoja na mwanajeshi wa Bahrain wameuawa katika shambulizi katika mpaka kati ya Saudi Arabia na Yemen, jeshi la Bahrain limesema huku ikiwashutumu waasi wa Houthi wa Yemen kwa shambulizi hilo.

https://p.dw.com/p/4Wnni
Mkuu wa Baraza la Juu la Siasa la waasi wa Houthi Mahdi al-Mashat akipeana amkono na afisa wa Omani walipokutana mjini Sanaa, Yemen Aprili 9, 2023. Hivi majuzi makundi hayo yalikuwa Saudi Arabia kwa mazungumzo ya kusaka amani.
Mkuu wa Baraza la Juu la Siasa la waasi wa Houthi Mahdi al-Mashat akipeana amkono na afisa wa Omani walipokutana mjini Sanaa, Yemen Aprili 9, 2023. Hivi majuzi makundi hayo yalikuwa Saudi Arabia kwa mazungumzo ya kusaka amani. Picha: SABA NEWS AGENCY/REUTERS

Taarifa ya jeshi imesema baadhi ya wanajeshi pia wamejeruhiwa katika shambulizi hilo la droni dhidi ya vikosi vya Bahrain kwenye mpaka wa kusini wa Saudi Arabia, licha ya kusitishwa mapigano kati ya makundi yanayohasimiana.

Ndege iliyo na watumishi wa afya ilipelekwa kwa ajili ya kuwahamisha majeruhi na kuirejesha miili Bahrain.

Vikosi vya Bahrain ni sehemu ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulioanzishwa Machi 2015, miezi kadhaa baada ya waasi wa Houthi kudhibiti mji mkuu wa Yemen, Sana'a na maeneo mengine, na kusababisha serikali ya Yemen kukimbia kuelekea kusini mwa mji wa Aden.