1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bajeti ya ulinzi ya Marekani na Erdogan ziarani Berlin

Oumilkheir Hamidou
15 Agosti 2018

Bajeti ya jeshi la Marekani, mkutano kati ya kansela Angela Merkel na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mjini Berlin na msiba wa kuvunjika daraja ya njia kuu mjini Genua nchini Italia magazetini.

https://p.dw.com/p/33Byp
Angela Merkel und Recep Tayyip Erdogan
Picha: picture-alliance/dpa/K. Ozer

Tunaanzia Marekani ambako rais Donald Trump anatunisha misuli kwa kutangaza bajeti kubwa ya ulinzi itakayofungua njia ya kubuniwa kikosi cha anga za juu, baada ya kikosi cha nchi kavu, baharini na angani. Dala bilioni 716 zitagharimu mpango huo. Una maana gani, linajiuliza gazeti la "Sächsische Zeitung"  na kuandika: "Bajeti hiyo iliyokithiri haimuingii yeyote akilini na hakuna pia sababu ya kuwa na bajeti kubwa kama hiyo ; si kwa upande wa kitisho kwa usalama wa taifa, sio kwamba silaha zimechakaa na wala si kwamba kuna upungufu wa silaha nyenginezo. Kisiasa uamuzi wake ni hatari, kijeshi ni wa uchukozi na kimaadili hakuna anaeweza kuutetea. Marekani inatoa ishara mbaya.

Hakuna asiyetambua nini hasa lengo halisi la bajeti hiyo ya juu kupita kiasi ya kijeshi. Kwa kufanya hivyo Trump anataka kuwashinikiza zaidi tu washirika wa Marekani wazidishe viwango vya bajeti zao za ulinzi. Mataifa mfano wa China na Urusi hayatopakata mikono na kukodowa macho. Kitakachofuata itakuwa kuzidishwa nguvu za kijeshi, kuzigeuza silaha ziwe za kimambo leo na kuongeza silaha: na hilo halitaifanya dunia iwe salama."

Erdogan anaweza kubadilisha msimamo wake

Gazeti la "Südwest Presse" linahofia mtindo wa Donald Trump wa kupenda kutunisha misuli usije ukaitumbukiza Marekani katika hali ya upweke.Tukitoka Marekani tunaelekea Uturuki ambako zahma iliyosababishwa na vikwazo vya Marekani inatishia kuvuruga shughuli ua kiuchumi za nchi hiyo, ambayo ni mshirika wa jadi wa jumuia ya kujihami ya NATO. Rais Recep Tayyip Erdogan anapanga kuitembelea rasmi Ujerumani ambako atakuwa na mazungumzo pamoja na kansela Angela Merkel. Kuhusu umuhimu wa ziara hiyo linaandika gazeti la "Leipziger Volkszeitung": "Mazungumzo atakayokuwa nayo Berlin yanaweza kumsaidia Erdogan kugundua vyanzo tofauti vya kiuchumi.

Miongoni mwa vyanzo hivyo ni ule ukweli kwamba cheo chake kama kiongozi mashuhuri wa Uturuki ya kimambo leo daima kimekuwa kikifungamanishwa na Umoja wa Ulaya. Ulaya ndiko zinakotokea fedha, wataalam na teknolojia inayotumika kuigeuza Uturuki iwe ya kimambo leo. Erdogan akitaka kuifuata tena njia hiyo,  njia ambayo daima inafuata mfumo wa taifa linaloheshimu sharia, basi anaweza kujikwamua toka mzozo huu wa sasa. Akitaka lakini kuendelea na sera yake bila ya kuujali Umoja wa ulaya, basi ataporomoka. Merkel atamuonyesha njia zote hizo, kama kawaida yake kwa utulivu na bila ya kinyongo."

Ajali ya Genua na miundombinu iliyochakaa Italia

Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Italia ambako msiba uliosababishwa na kuvunjika daraja katika mji wa Genua umeangamiza maisha ya watu wasiopungua 37 na wengine wasiojulikana idadi kujeruhiwa. Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika: "Miundo mbinu iliyochakaa ya Italia imekuwa daima ikiwakosesha usingizi wataalam wa usafiri nchini humo. Maonyo yamekuwa yakipuuzwa na serikali nyingi zilizoingia madarakani nchini Italia. Badala ya kuzifanyia ukarabati daraja na njia za chini ya ardhi zilizochakaa, mawaziri wa usafiri  mjini Roma walikuwa wakizungumzia kuhusu upungufu wa fedha."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman