Bajeti za kijeshi zapungua
17 Aprili 2012Kwa mujibu wa ripoti ya SIPRI iliyotolewa leo, fedha zilizotumika kwa ajili ya shughuli za kijeshi kwa mwaka 2011 zilifikia kiasi cha dollar trillioni 1.74. za Kimarekani. Mwaka hadi mwaka, bajeti ya kijeshi imekuwa ikipanda katika mataifa mengi lakini sasa mgogoro wa kimataifa wa fedha umeziathiri nchi nyingi na hivyo kuzilazimisha kubana matumizi hata katika ununuzi wa silaha. Ujerumani, Ufaransa, Brazil na Uingereza ni miongoni mwa nchi zilizopunguza bajeti ya kununua silaha.
Carina Solmirano kutoka taasisi ya SIPRI anatabiri kwamba Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zitaendelea kupunguza bajeti hiyo hata katika miaka inayokuja. Lakini nchi kama Brazil ina sababu tofauti ya kupunguza bajeti ya jeshi. "Brazil nayo ilipunguza bajeti yake ya kijeshi mwaka 2011 licha ya kwamba ilikuwa ikiiongeza bajeti hiyo kwa karibu miaka 10 iliyopita," anaeleza Solmarino. "Lakini Brazil ilifanya hivyo ili kupunguza ukuaji wa kiuchumi na kuzuia mfumuko wa bei."
China na Urusi zaongeza bajeti
Nchini Urusi pameonekana kuwa na mabadiliko tofauti: Taasisi ya SIPRI imebaini kwamba mwaka jana nchi hiyo iliongeza bajeti yake ya kijeshi kwa asilimia 9.7. Serikali ya Urusi ilitumia karibu dollar billioni 72 za Kimarekani kununua silaha na hivyo kuiweka nchi hiyo katika nafasi ya tatu kati ya nchi zenye bajeti kubwa kabisa ya kijeshi. Nchi inayoongoza kwa matumizi makubwa ni Marekani ikifuatiwa na China. Ufaransa inashika nafasi ya nne ikifuatiwa na Uingereza.
China nayo inataka kuongeza zaidi na zaidi fedha kwa ajili ya kununulia silaha. Mwaka jana, serikali ya nchi hiyo iliongeza kiasi hicho cha fedha kwa asilimia 6.7 ikilinganishwa na mwaka 2010. Na kwa mwaka huu China imelenga kuwa na ongezeko la asilimia 11.2 katika bajeti yake ya kijeshi. Nchi za Magharibi zimetiwa wasiwasi na uamuzi huo. Hata hivyo Gu Xuewu, ambaye ni mkurugenzi wa kituo cha masuala ya kimataifa katika chuo kikuu cha Bonn, Ujerumani, anaeleza kwamba hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi. Kwa mtazamo wake, ongezeko katika bajeti ya kijeshi linaendana na ukuaji wa kiuchumi wa China kwani wakati huu China inaongeza matumizi katika karibu kila sekta.
Mwandishi: Hartert-Mojdehi, Sabine / Mikhail Bushuev / Cao Haiye
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhairi: Saumu Yusuf