Balozi wa Urusi nchini Uturuki auliwa Ankara
19 Desemba 2016Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Urusi imesema katika taarifa iliyotangazwa na shirika la habari la serikali, TASS, kwamba balozi Karlov ameuliwa. Ufyetuaji risasi umetokea katika ukumbi wa sanaa wa Cagdas Sanatlar Merkezi, katika wilaya ya Cankaya mjini Ankara ambako kuna balozi nyingi za kigeni, ukiwemo ubalozi wa Urusi.
"Leo ni siku ya huzuni kubwa kwa diplomasia ya Urusi," amenukuliwa akisema msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje, Marian Zakharova. "Leo mjini Ankara kutokana na kushambuliwa ubalozi wa Urusi nchini Uturuki, Andrey Karlov, amepata majeraha mabaya ambayo yamesababisha kifo chake. Tunalichukulia tukio hili kama shambulizi la kigaidi," akaongeza kusema Bi Zakharova. Urusi imeapa kulipiza kisasi mauaji ya mwanadiplomasia wake.
Vyombo vya habari vya Uturuki vimeripoti kuwa Karlov, aliyakuwa na umri wa miaka 62, alikuwa akitoa hotuba katika maonyesho ya sanaa ya picha yaliyodhaminiwa na Urusi wakati alipopigwa risasi mgongoni. Gazeti la Uturuki, Hurriyet, limemnukuu mpigapicha aliyekuwa katika eneo la tukio akisema mshambuliaji aliyekuwa amejihami na bunduki alipiga kelele akitoa kauli za kidini na kuzungumzia kuhusu hali katika mji wa Syria ulioharibiwa na vita wa Aleppo.
Muuaji ni polisi, alipiza kisasi mauaji ya Aleppo
Mkanda wa video umeonyesha mwanamume aliyevalia suti nyeusi na tai akiwa na bunduki mkononi na akionyesha ishara hewani katika ukumbi wa maonyesho hayo ya sanaa. Alikuwa afisa wa polisi ya kupambana na fujo mwenye umri wa miaka 22 ambaye alikuwa katika mapumzika siku ya maonyesho hayo, lakini akajifanya kuwa mlinzi wa balozi Karlov na kufaulu kuingia ukumbini. Shirika la habari la serikali ya Uturuki Anadolu limesema mshambuliaji huyo ameuawa katika operesheni ya polisi, bila kutoa maelezo zaidi. Meya wa mji wa Ankara amemtambua mshambuliaji kama afisa wa polisi wa Uturuki.
Utawala wa Urusi Kremlin umefahamishwa kuhusu hujuma hiyo. Rais wa Urusi, Vladmiri Putin, amezungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, kuhusu mauaji ya balozi Karlov. Karlov alizaliwa mjini Moscow mnamo mwaka 1954. Mwanadiplomasia huyo alianza kazi yake chini ya utawala wa muungano wa zamani wa Sovieti mwaka 1976. Aliwahi kuwa balozi wa Urusi nchini Korea Kaskazini kati ya mwaka 2001 na 2006.
Mauaji hayo yametokea baada ya siku kadhaa za maandamano nchini Uturuki kuhusu jukumu la Urusi nchini Syria, ingawa Urusi na Uturuki zinashirikiana kuwaondosha raia kutoka mji ulioharibiwa na vita wa Aleppo.
Karlov amekufa kutokana na majeraha ya risasi baada ya kushambuliwa, siku moja kabla kufanyika mkutano wa pande tatu kati ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu na mwenzao wa Iran, Mohammad Javad Zarif kuhusu mzozo wa Syria mjini Moscow.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ameyalaani vikali mauaji ya balozi Karlov nchini Uturuki na kuonyesha mshikamano na Urusi. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataia, Samantha Power, pia amejiunga na viongozi wengine kuyalaani mauaji hayo.
Mwandishi:Josephat Charo/afpe/reuters/dpa
Mhariri:Mohammed Khelef