Marekani zaonya kuhusu mashambulizi Uganda na Tanzania
20 Juni 2019"Kuna fununu za uwezekano wa mashambulizi katika maeneo yanayotembelewa zaidi na wataalamu wa kigeni ndani ya Afrika Mashariki, ikiwemo Uganda," ulisema ubalozi wa Marekani nchini Uganda siku ya Alhamisi, siku moja baada ya ubalozi mjini Dar es Salaam kutoa tahadhari sawa ya kiusalama.
Tahadhari zote mbili hazikuwa na ushahidi madhubuti wa kitisho hicho au taarifa kuhusu muda," lakini zilisema watu wanapaswa kuepuka kuka kwenye makundi na kukaa chonjo.
Wakati Uganda na Tanzania hazikabiliwi na mashambulizi ya mara kwa mara kama Kenya - ambayo inalengwa mara kwa mara na mashambulizi mabaya ya kundi la Al-Shabaab la nchini Somalia - hazikajuwa na kinga.
"Mwaka 2010 kulikuwa na mashambulizi mjini Kampala kwenye eneo la kutazamia fainali ya kombe la dunia ambamo watu zaidi ya 70 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Al-Shabaab ilidai kuhusika .. na kutishia kufanya mashambulizi zaidi katika eneo hilo," Inasema Uingereza kwenye ukurasa wake rasmi wa usafiri.
Kwa Tanzania, Uingereza inasema kwamba "magaidi wanaweza kujaribi kufanya mashambulizi," lakini kwamba Tanzania haijakumbwa na tukio lolote kubwa la kigaidi tangu mashambulizi ya ubalozi wa Marekani mnamo mwaka 1998.
Tanzania: Polisi wetu wako kazini
Waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Kangi Lugola amewatoa hofu raia kwa kusema kuwa nchi hiyo iko salaama na kuwataka waendelea na shughuli zao za kawaida.
Lugola alisema taarifa zilizotolewa na ubalozi wa Marekani zinachukuliwa kama taarifa nyingine za kawaida na kwa maana hiyo hakuna sababu ya watu kuingia katika hofu kwa vile vyombo vya usalama viko kazini wakati wote.
"Hizi ni sehemu ya taarifa za kawaida, ambapo kama wenzetu wameweza kuzipata, na tumeweza kuwasiliana nao kupitia jeshi la polisi, niwahakikishie Watanzania kwamba wasiwe na hofu, wala wasiwe na wasiwasi. Vyombo vya usalama vinaendelea kufanya kazi yake," amesema waziri huyo na kuongeza kuwa tahadhari ya kiusalama ni ya kawaida.
Hata hivyo, taarifa hiyo ya ubalozi wa Marekani haikufahamisha ni watu gani wanaokusudia kufanya shambulizi hilo na wala haikueleza muda na siku mbali ya kuwataka wananchi kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.
Alipoulizwa na vyombo vya habari kuhusiana na tishio hilo muda mfupi baada ya onyo la ubalozi wa marekani, Mkuu wa jeshi la polisi IGP, Simon Sirro alikiri jeshi hilo lilifahamu kuhusu jambo hilo siku moja kabla na alisema vikosi vyake vilikuwa viko kazini.
Hata hivyo, mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda alitumia mtandao wake Jumatano usiku kukanusha kuhusu tishio hilo.
Vyanzo: Mashirika/George Njogopa amechangia kwenye ripoti hii.