1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban aonya juu ya hali ya kisiasa ya Kongo

Admin.WagnerD6 Julai 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameonya kuwa hali ya sasa kisiasa kuelekea uchaguzi ujao wa urais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaweza kupelekea kuibuka kwa mgogoro mkubwa .

https://p.dw.com/p/1JJyu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha: Getty Images/AFP/Y. Kontarinis

Katika ripoti iliyowasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema huenda majeshi ya kulinda amani nchini Kongo yakalazimika kuomba msaada kutoka Umoja wa Mataifa.

" Kukosekana kwa utashi wa kisiasa na kutokuwepo kwa majadiliano yenye tija miongoni mwa wadau wa kisiasa nchini Kongo basi hofu inayoibuka kuhusiana na majaliwa ya kufanyika kwa uchaguzi huo inaweza kuibua vurugu na kuondoa hali ya utulivu katika taifa hilo " alisema Katibu Mkuu Ban Ki-moon.

Tayari serikali ya Kongo imekwisha sema kuwa kuna uwezekano uchaguzi huo usifanyike mwezi Novemba kama inavyotarajiwa kutokana na sababu zinazohusiana na matatizo ya usambazaji wa vifaa vya uchaguzi lakini mahasimu wa kisiasa wa Rais Joseph Kabila wamekuwa wakimshutumu na kusema madai hayo yana lengo la kumuwezesha kujaribu kusalia madarakani. Hata hivyo serikali ya Kongo imekanusha madai hayo.

Katiba yambana Rais Kabila

Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001, anabanwa na katiba kutowania muhula wa tatu wa uongozi ingawa washirika wake wameonesha nia ya kutaka kuwepo na kura ya maoni nchini humo yanye lengo la kumuwezesha kuwania tena nafasi hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila.Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Wakosoaji kadhaa wa Rais Kabila wametiwa mbaroni tangu mwaka jana hatua ambayo Umoja wa Mataifa na makundi ya wanaharakati yanasema ina lengo la kudhibiti baadhi ya wanasiasa wenye sifa stahiki katika mchakato wa kuelekea uchaguzi huo.

Watu kadhaa waliuawa wakati wa maandamano yaliyofanyika Januari 2015 kupinga hatua ya marekebisho ya kipengele kimoja wapo cha katiba ya nchi hiyo kwa lengo la kusogeza mbele uchaguzi huo.

Jeshi la kulinda amani nchini Kongo MONUSCO linapanga mikakati ya kukabiliana na vurugu zinazoweza kujitokeza wakati wa mchakato kuelekea uchaguzi huo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufahamishwa kuhusiana na hali hiyo ya sasa ya kisiasa nchini Kongo .

Hatua ya kuondoa madarakani utawala wa aliyekuwa Rais wa Kongo Mobutu Sese Seko mnamo mwaka 1997 ilipelekea kuibuka kwa mgogoro nchini humo uliosababisha vifo vya mamilioni ya watu hali iliyo lazimu kuwepo kwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa mataiafa nchini humo tangu mwaka 2000.

Mwandishi : Isaac Gamba/ RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga