Ban Ki Moon aahidi msaada kwa wahanga wa tetemeko la ardhi
24 Mei 2008BEIJING
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon ametembelea eneo la kusini magharibi ya China lililoathirika zaidi na tetemeko la ardhi na ameahidi kuwasaidia wahanga.Katibu mkuu aliwasili katika mji mkuu wa jimbo la Sichuan,Chengdu hii leo siku moja baada ya ziara yake nchini Myanmmar ambako alifanikiwa kuushawishi utawala wa kijeshi wa nchi hiyo kuwaruhusu wafanyikazi wa misaada wa kimataifa kuingia nchini humo kuwasaidia manusura.Aidha katibu mkuu amekutana na waziri mkuu wa China Wen Jiabao mjini Yingxiu ambako ndio kitovu cha tetemeko la ardhi kwenye jimbo hilo la Sichuan ambako watu zaidi ya elfu 80 walikufa au kutoweka.China imesema kwamba kiasi cha watu millioni tano na nusu wameachwa bila makaazi kufuatia janga hilo na zaidi ya watu millioni 11 wanatazamiwa kupatiwa makaazi katika makambi ya wakimbizi kufuatia hatari iliyopo kwenye maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi ambako watu wanaondolewa.