1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban ki moon afungua kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

Halima Nyanza23 Septemba 2010

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon leo amekifungua kikao cha 65 cha cha baraza kuu la umoja huu, kwa kuelezea masuala yatakayojadiliwa na ufumbuzi utakaopatikana kuanzia mabadiliko ya hali ya hewa hadi uchumi.

https://p.dw.com/p/PLAK
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha: AP

Akifungua kikao hicho leo katika Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amezungumzia changamoto inayoikabili dunia kuhusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Amesema miaka mitatu iliyopita mabadiliko ya hali ya hewa yalielezwa kwamba ni changamoto kubwa kwa wakati huu na kwamba bado tatizo hilo limebaki kuwa kubwa mpaka hivi sasa.

Aidha amesema kwamba ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu duniani itaongezeka kwa asilimia 50, na kwamba kutokana na ongezeko la idadi ya watu duniani ni dhahiri kuna hitajika kupunguzwa utoaji wa gesi inayoharibu mazingira kwa asilimian 50 ,ifikapo mwaka huo.

Na katika hatua nyingine, Rais wa Marekani Barack Obama akizungumza katika mkutano huo  amesema nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo ya kidiplomasia na Iran, lakini lazima taifa hilo la kiislamu lithibitishe kwamba mpango wake wa nyuklia ni wa amani.

Akizungumza katika mkutano huo wa baraza kuu la umoja wa mataifa muda mfupi uliopita, amesema Marekani na Jumuia ya Kimataifa zinatafuta ufumbuzi juu ya tofauti zao na Iran.

Aidha akizungumzia kuhusiana na Mapambano dhidi ya mtandao wa kigaidi wa al Qaeda na Taliban, Rais Obama amesema nchi yake inaendeleza mapambano dhidi ya mtandao huo wa kigaidi.

Ameiambia hadhara iliyohudhuria mkutano huo kwamba majeshi ya Marekani na washirika wake yanafanya kazi kuweza kuvunja nguvu ya Taliban nchini Afghanistan na kuiandaa serikali ya Afghanistan kuanza kushika majukumu kwa ajili ya kulinda usalama mwaka ujao nchini humo.

Aidha amesema nchi yake pia inafanya kazi kuweza kuepusha silaha za nyuklia kuangukia katika mikono ya watu wenye misimamo mikali.

Kuhusu Mashariki ya kati, alitoa wito akiitaka jumuiya ya kimataifa iunge mkono juhudi zake za  kumaliza  hali ya mkwamo kuhusiana na mazungumzo ya amani ya eneo hilo, akionya kwamba damu zaidi itamwagika pindi juhudi hizo zitashindwa.

Amesema pia kwamba uchumi wa dunia unaimarika, kutokana na msukosuko wa kiuchumi ulioikumba dunia.

Mkutano huo unafanyika kufuatia majadiliano ya siku tatu katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali ya kijamii duniani chini ya mpango unaojulikana kama malengo ya maendeleo ya milenia.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,cnn)

Mhariri: Abdul-Rahman