Ban Ki-moon aitaka Syria kuruhusu misaada ya kiutu
3 Machi 2012Wakati dunia ikiendelea kukasirishwa na utawala wa Syria, kundi linaloangalia hali nchini humo limeripoti kuwa kiasi ya watu 38 wameuwawa siku ya Ijumaa, ikiwa ni pamoja na watu 10 waliopigwa risasi na kufariki katika eneo la Baba Amr,wilaya ambayo ni ngome kuu ya waasi katika mji wa Homs, ambayo inadhibitiwa sasa na majeshi ya serikali kuanzia siku ya Alhamis.
Waandishi washambuliwa
Wakati huo huo mpiga picha raia wa Uingereza Paul Conroy , ambaye alitolewa kwa njia za siri kutoka Homs kupitia Lebanon , amesema wakati akiwa hospitalini nchini Uingereza kuwa mashambulio ya makombora yaliyofanywa na majeshi ya serikali kwa muda wa mwezi mmoja dhidi ya mji huo yalikuwa ni mauaji ya kiholela , na kuna maelfu ya watu ambao wanasubiri tu kufa.
Mwandishi habari kutoka Ufaransa Edith Bouvier , mwenye umri wa miaka 31 na mpiga picha William Daniels , mwenye umri wa miaka 34, ambao wamewasili mjini Paris siku ya Ijumaa baada ya kutolewa kwa njia za siri nao kutoka Syria, wamesema kuwa utawala wa nchi hiyo unaonekana kulenga vyombo vya habari vya kigeni katika eneo la Baba Amr katika wimbi la mashambulio ambayo yameuwa waandishi wawili.
Waandamanaji waomba msaada
Hata hivyo maelfu ya watu walimiminika mitaani mjini Damascus na mji wa pwani wa Aleppo siku ya Ijumaa wakihimiza mataifa ya magharibi kuwapa waasi silaha, na kusababisha majeshi ya serikali kufyatua risasi, wameeleza wanaharakati na wachunguzi nchini humo.
Mjini New York , katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon ameitaka Syria bila masharti kuruhusu misaada ya kiutu. Maafisa wa Syria ni lazima wafungue njia bila ya kuweka masharti ili jamii zipatiwe misaada, amesema Ban katika mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya umoja wa mataifa.
Haikubaliki kabisa, na haivumiliki. Ni kwa vipi binadamu anaweza kuvumilia hali hii, amesema. Lakini Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Ja'afari amemshutumu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kile alichokiita kuitusi serikali ya Rais Bashar al-Assad kutokana na matamshi yake ya kuwakandamiza kinyama waandamanaji wa upinzani.
Marekani yamuonya Assad
Marekani imezitaka nchi zote kushutumu unyama wa kutisha unatokea nchini Syria wakati Rais Barack Obama ametangaza kuwa siku za Assad zinahesabika.
Kwa upande wake Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amesema kuwa kile kinachoendelea nchini Syria ni kashfa kubwa. Kuna zaidi ya watu 8,000 waliouwawa, mamia ya watoto waliouwawa, na mji wa Homs unakabiliwa na hatari ya kufutwa kabisa katika ramani.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/rtre
Mhariri: Bruce Amani.