1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki Moon alaani mashambulizi mapya Syria

7 Aprili 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameishutumu vikali serikali ya Syria kwa mashambulizi yake ya hivi karibuni dhidi ya raia. Ban ameitaka Syria kutimiza ahadi yake ya kusitisha operesheni zote za kijeshi.

https://p.dw.com/p/14Z99
Syrian youth stand in a building damaged by tank shells in a neighborhood of Damascus, Syria, after a raid by Syrian troops killed several rebels and civilians Thursday, April 5, 2012. Syrian troops launched a fierce assault Thursday, days ahead of a deadline for a U.N.-brokered cease-fire, with activists describing it as one of the most violent attacks around the capital since the year-old uprising began. (Foto:AP/dapd)
Syrien Bürgerkrieg Zerstörungen in DamaskusPicha: dapd

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya habari ya Katibu huyo Mkuu, Ban amesema inasikitisha kuona vikosi vya Syria vikiwashambulia raia wasio na hatia, wakiwemo wanawake na watoto, licha ya ahadi za serikali za kutisitisha matumizi ya silaha nzito katika maeneo ya makaazi.

Ban alisema muda wa mwisho wa tarehe kumi Aprili wa kutimiza utekelezaji wa serikali – kusitisha mapigano na kuviondoa vikosi, jinsi ilivyoidhinishwa na Baraza la Usalama, sio sababu ya kuendelea kufanya mauaji.

Vifo zaidi yaripotiwa

Wanaharakati wa upinzani wanasema takriban watu 27 wakiwemo wanajeshi wa Syria, waasi na raia waliuwawa katika mchafuko Ijumaa (6 Aprili 2012), ikiwa ni siku nne kabla ya muda huo wa mwisho wa Aprili 10 wa kusitisha matumizi ya zana nzito na kuyaondoa majeshi uliokubaliwa na Rais Bashar al-Assad kama sehemu ya mpango wa amani unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Kofi Annan akiwa na Ban Ki Moon mjini New York
Kofi Annan na Ban Ki Moon wanaendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa SyriaPicha: dapd

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu Kofi Annan alisema serikali na upinzani ni lazima wasitishe mapigano saa kumi na mbili asubuhi saa za nchini humo mnamo tarehe 12 mwezi huu wa Aprili, ikiwa serikali ya Syria itatimiza muda wake wa mwisho saa 48 mapema, kuviondoa vikosi kutoka mijini na kusitisha matiumizi ya silaha kali.

Taarifa ya Ban iliendelea kusema kuwa serikali ya Syria inasalia kuwajibika kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu pamoja na sheria ya kimataifa, na hayo ni lazima yasitishwe mara moja. Braza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo China na mshirika mkubwa wa Syria Urusi, Alhamisi (05 Aprili 2012) waliidhinisha kwa pamoja muda wa mwisho uliopendekezwa kuumaliza mzozo wa Syria na wakaoinya nchi hiyo kuwa wangetathmini hatua nyingine ikiwa haitatimiza mapendekezo hayo.

Wakimbizi wa Syria wafurika Uturuki

Wakati hali ikizidi kuwa mbaya nchini Syria, maelfu ya wakimbizi walimiminika mpakani na kuingia nchini Uturuki, wakiwa na hadidhi tofauti za mauaji ya kikatili, makaburi ya pamoja na majumba yaliyochomwa.

Idadi ya wakimbizi wa Syria wanaotorokea Uturuki yaongezeka
Kofi Annan na Ban Ki Moon wanaendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa SyriaPicha: Reuters

Idadi ya Wasyria wanaokimbilia Uturuki imepanda katika katika siku za hivi karibuni huku kiasi ya theluthi moja ya jumla ya wakimbizi 24,000 wakiwasili nchini humo katika wiki mbili zilizopita.

Takriban wakimbizi 2,500 walivuka mpaka huo Alhamisi pekee, kulingana na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uturuki Ahmet Davutoglu, akiongeza kuwa idadi ya kila siku ya wale wanaoingia imeongezeka marambili tangu Syria ilipoahidi wiki iliyopita kuheshimu mpango wa kusitisha vita.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Mohamed Khelef