1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki-moon ataka kipindi cha mpito Libya

8 Julai 2011

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amezungumza na uongozi wa Libya juu ya hatua za kumaliza mapigano ya sasa, huku Baraza la Wawakilishi la Marekani likikataa jeshi lake kushirikiana na waasi wa Libya.

https://p.dw.com/p/11rO3
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: AP

Msemaji wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba Ban Ki-moon alizungumza na Waziri Mkuu wa Libya, Al-Baghdadi Ali Al-Mahmoudi, jioni ya jana (7 Julai 2011) kwa njia ya simu, na kwamba mazungumzo yao yalijikita kwenye umuhimu wa kuvizuia vita vinavyoendelea kati ya waasi na vikosi vitiifu kwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.

Kupitia mazungumzo hayo, serikali ya Libya imemkubalia mjumbe maalum wa Ban Ki-moon kwa nchi hiyo, Abdullah Al-Khatib, kutembelea mji mkuu wa Tripoli kwa mashauriano ya haraka juu ya maafa dhidi ya binaadamu yanayosababishwa na vita hivyo, na kuufanyia kazi mpango utakaoruhusu kuwepo kwa kipindi cha mpito kuelekea amani ya kudumu kwa Walibya wote.

Baraza la Wawakilishi la Marekani laizuia Pentagon

Seneta John McCain wa Republican ni muungaji mkono wa waasi wa Libya
Seneta John McCain wa Republican ni muungaji mkono wa waasi wa LibyaPicha: AP

Huku hayo yakiendelea, Baraza la Wawakilishi la Marekani limekataa pendekezo la kuzuia fedha za nchi hiyo kutumika kwenye operesheni ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO nchini Libya, lakini likapigia kura ya kuizuia nchi hiyo kushirikiana kwa namna yoyote na waasi wa Libya.

Wajumbe 225 walipiga kura za kuikataza Marekani kujihusisha moja kwa moja na vita vya Libya, huku wengine 201 wakiunga mkono.

Mwakilishi wa jimbo la Oklahoma kutoka chama cha Republican, Tom Cole, ndiye aliyeliwasilisha hatua hizo kwenye Baraza la Wawakilishi, akisema kwamba Wamarekani "hawafurahishwi na namna Rais Barack Obama anavyouchukulia mgogoro wa Libya".

Katazo hilo la Baraza la Wawakilishi linasomeka kwamba: "Makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon, hayatakiwi kutoa vifaa vya kijeshi, mafunzo au ushauri, au msaada wowote kwa shughuli za kijeshi, kwa kundi lolote au mtu, au kwa sehemu ya vikosi vyenye silaha vya Libya, kwa dhamira ya kusaidia kundi au mtu kuendesha harakati za kijesha ndani au dhidi ya Libya".

McCain asema Baraza la Wawakilishi limepotosha

Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

Hata hivyo, Seneta John McCain wa chama cha Republican, ambaye ni muungaji mkono mkubwa wa waasi wa Libya, ameiita kura hii ya Baraza la Wawakilishi kuwa ni "ya kuudhi", akisema kwamba "inatuma ujumbe wenye upotofu kwa Gaddafi na kwa wale wanaopigania demokrasia nchini Libya".

Kura hii imekuja katika wakati ambapo Poland, ambayo inashikilia uraisi wa Umoja wa Ulaya kwa sasa, ikisema imeanzisha ushirikiano wa kibalozi na Baraza la Mpito la Kitaifa, chombo cha kisiasa cha waasi wa Libya, kwa kumuweka balozi wake kwenye ngome ya waasi hao, kwenye mji wa mashariki ya Libya wa Benghazi.

Wiki iliyopita, Ufaransa ilisema kwamba iliwapa waasi kile ilichokiita "silaha za kujilinda wenyewe", ikidai huko ni kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa.

Ufaransa inasema ilichukuwa hatua hiyo baada ya kuliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Miongoni mwa silaha hizo ni bunduki za kawaida na mizinga ya kurushia maroketi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/Reuters
Mhariri: Othman Miraji