1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki Moon ataka machafuko Syria yakome

7 Januari 2012

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali inayoendelea kuzorota nchini Syria. Ni kufutia shambulizi la bomu la mtu wa kujitoa muhanga ambapo watu 26 waliuwawa mjini Damascus.

https://p.dw.com/p/13fjN
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/dpa

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon pamoja na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali nchini Syria. Ban amesema katika taarifa yake kwamba machafuko yote yanayoendelea nchini humo hayakubaliki na lazima yakome. Upinzani wa Syria umeulaumu utawala wa rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad, kwa kuushambulia kwa bomu mji mkuu Damascus. Mshambuliaji wa kujitoa muhanga alijilipua mwenyewe karibu na shule moja jijini humo na kusababisha vifo vya watu 26 hapo jana Ijumaa (05.01.2012).

Katika taarifa yake kwa vyombo vya harabi, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelieleza shambulio hilo kuwa ni kitendo cha kinyama na kutoa risala za rambirambi kwa walioathiriwa. Baraza hilo kwa mara nyengine tena linatarajiwa kufutilia suala la vikwazo dhidi ya Syria katika kikao chake Jumanne wiki ijayo ijayo. Hata hivyo Marekani ina wasiwasi kama mkutano huo utafikia uamuzi wa maana.

China na Urusi, ambazo ni nchi wanachama wa kudumu katika baraza la usalama na ambazo zina kura ya turufu, zimekuwa zikipinga azimio la kulaani machafuko nchini Syria. Lakini baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura mwezi Desemba mwaka jana kulaani ukiukaji wa haki za binaadamu unaofanywa Syria.

Mjini Washington, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani, Victoria Nuland, amedokeza kwamba azimio dhidi ya Syria halitarajiwi kufikiwa hivi karibuni. "Nadhani hii itakuwa hatua inayofuata katika mashauriano. Sina uhakika kwamba tunatarajia kukamilisha chochote katika mkutano wa Jumanne ijayo," alisema Nuland wakati alipozungumza na waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 6,000 wameuwawa kwenye machafuko kati ya wanaharakati wanaopigania mageuzi na vikosi vya serikali ambayo yalianza mwezi Machi mwaka jana.

Mwandishi: Josephat Charo/DPAE

Mhariri: Sudi Mnette