1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban Ki Moon azionya Iran na Israel

18 Agosti 2012

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amemshutumu vikali kiongozi wa kidini wa Iran pamoja na Rais wa nchi hiyo akiyataja matamshi yao ya karibuni dhidi ya Israel kuwa ni ya "kukera na uchochezi".

https://p.dw.com/p/15sBr
epa03088377 UN Secretary-General Ban Ki-moon speaks during a joint press conference with the Palestinian Authorities President Mahmoud Abbas (unseen) in the West Bank town of Ramallah on 01 February 2012. UN Secretary-General Ban Ki-Moon kicked off a series of meetings 01 February with Israeli and Palestinian leaders, holding talks in Jerusalem with President Shimon Peres. EPA/ATEF SAFADI
Palästina UN Generalsekretär Ban Ki-moon Gazastreifen Israel PressekonferenzPicha: picture-alliance/dpa

Maelfu ya WaIran walipiga kelele wakisema "kifo kwa Marekani, kifo kwa Israel" wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na serikali Ijumaa (17.08.2012) naye Rais Mahmoud Ahmadinejad akawaambia kuwa hakuna nafasi ya taifa la kiyahudi katika mustakabali wa Mashariki ya Kati.

Ofisi ya Habari ya Umoja wa Mataifa imesema Katibu Mkuu Ban Ki Moon amekasirishwa na matamshi hayo yanayoitishia Israel. Taarifa hiyo imesema Ban anawataka viongozi katika kanda hiyo kutumia sauti zao kwa wakati huu kupunguza, badala ya kuongeza hofu.

Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad anasema mpango wake ni wa nyuklia ni wa amani pekee
Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad anasema mpango wake ni wa nyuklia ni wa amaniPicha: AP

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa, wanachama wote ni lazima waepuke kutoleana vitisho au matumizi ya nguvu dhidi ya uadilifu wa himaya au uhuru wa kisiasa wa nchi yoyote.

Mapema wiki hii, vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa Kiongozi wa Kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema Israel siku moja itarejeshwa kwa taifa la Palestina na isahaulike kabisa.

Matamshi hayo ya Iran yalikuja wakati kukiwa na uvumi kutoka kwa vyombo vy ahabari vya Israel kuwa nchi hiyo inapanga kuvishambulia viwanda vya nyuklia vya Iran kabla yan uchaguzi wa rais wa Marekani mwezi Novemba mwaka huu.

Wakati huo huo, aliyekuwa naibu wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema ijumaa (17.08.2012) kuwa shambulizi lolote dhidi ya Iran kuhusiana na mpango wake wa nyuklia linaweza kuingiza Israel katika vita vya maafa.

Shaul Mofaz, ambaye ni kiongozi wa upinzani bungeni, aliyejiuzulu kutoka baraza la mawaziri la Netanyahu mwezi uliopita ambako alihudumu kama makamu wa Waziri Mkuu, alisema kwenye televisheni ya Israel kuwa anahisi Israel inapanga tukio la pupa, na la kutowajibika.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanjahu ameapa kuilinda nchi dhidi ya mashambulizi
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanjahu ameapa kuilinda nchi yake dhidi ya mashambuliziPicha: dapd

Israel, Marekani na washirika wao barani Ulaya na kwingineko wanaamini kuwa Iran inatengeneza silaha za atomiki, madai ambayo Iran inakanusha ikisema mpango wao wa nyuklia ni wa amani.

Netanyahu anakasirishwa kuwa hatua za kidiplomasia za nchi za Magharibi za kujaribu kuilazimu Iran kusitisha mpango wake kufikia sasa zimekosa kufaulu. Duru za kijasusi zinadokeza kuwa Iran imekuwa ikiongeza kasi badala ya kupunguza mpango wake hali inayoongeza hofu.

Hata hivyo maafisa wa ngazi ya juu wa Israel wanasema uamuzi wa mwisho kuhusu ikiwa nchi hiyo itaishambulia Iran haujachukuliwa, huku mawaziri wakishindwa kukubaliana kuhusu suala hilo nao uongozi wa kijeshi haujafurahia uwezekano wa kushambulia kivyake bila uungaji mkono kikamilifu wa Marekani.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Sekione Kitojo