Ban Ki-moon kukamilisha jumatano ziara ya siku mbili Ujerumani
16 Julai 2008Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki -moon,ambaye baado yuko hapa Ujerumani kwa ziara rasmi ya siku mbili amesema kuwa ametiwa moyo na ubadilishanaji wafungwa kati ya Israel na wapiganaji wa Hezbollah wa nchini Lebanon.
Ubadilishanaji huo umeanza rasmi leo jumatano.
Kauli hiyo kinara wa Umoja wa Mataifa ameitoa jumatano mjini Berlin mbele ya waandishi habari.
Akiwa katika siku yake ya pili na ya mwisho ya ziara yake rasmi nchini Ujerumani ambayo aliianza jumanne,Ban Ki Moon amewambia waandishi habari kuwa amevutiwa na hatua hiyo ya kubadilishana kile alichoita "wafungwa".
Ameongeza kuwa ni matarajio yake kuwa huu ndio mwanzo wa matukio mengi yatakayofuatia hapo baadaye.
Amesifu mchango wa afisa wa kijerumani alieteuliwa na Umoja wa Mataifa kushughulikia suala hilo ambapo amekuwa kitembelea pande zote husika kwa kipindi cha miazi 18 ili kufanikisha kubadilishana huko.
Ameendelea kuwa anaomba kutapatikana ufumbuzi wa haraka wa suala la mwanajeshi mmoja wa Israel aliechukuliwa mateka na wapiganaji wa Kipalestina wanaoegemea kundi la Hamas.
Katibu mkuu huyo, ambae anakamilisha safari yake hii ya Ujerumani leo baada ya kutembelea ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko hapa mjini Bonn,akiwa baado mjini Berlin, alikanusha madai kuwa alionyesha wasiwasi kuhusu kutolewa kwa waranti wa kukamatwa rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan kuhusiana na mauaji ya halaiki ya Darfur.
Katika mahojiano yaliyochapishwa leo na gazeti la hapa Ujerumani la Sueddeutsche Zeitung, ameyaita kama "uongo mtupu", madai ya redio ya Sudan kuwa Ban Ki-moon alionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hatua ya mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ya ICC.
Amefafanua msimamo wa Umoja wa mataifa kuhusu uhuru wa mahakama hiyo akisema uamuzi wake ni lazima uheshimiwe.
Ameongeza kuwa mapendekezo kuwa aliidhalilisha mahakama ya kimataifa kama "yasiyokubalika" na kuongeza kuwa alieleweka vibaya.
Hata hivyo amesema kuwa endapo rais Bashir atashtakiwa hali hiyo itamuweka katika nafasi ngumu.
Ban Ki moon jana alikutana na Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel mjini Berlin na kujadilia masuala mbalimbali.
Ban Ki-moon ni katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa nane. Akiwa raia wa Korea Kusini ndie raia wa kwanza wa bara Asia kuchukuwa wadhifa huo baada ya kipindi cha miaka zaidi ya 30.
Alichaguliwa kuchukua ofisi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake Koffi Annan, kutoka Ghana Afrika,Oktoba mwaka 2006 na kuanza kazi rasmi mapema mwaka jana.
Kwa kuwa ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Ujerumani inapatikana hapa mjini Bonn,ndio maana imembidi afike hapa kuona vijana wake wanavyochapa kazi,kabla ya kuondoka kuelekea kwingine.