Bangi ruksa kwa wagonjwa Ujerumani
23 Julai 2014Kupamba moto kwa chuki dhidi ya Uyahudi kutokana na mzozo Gaza,suala la mzozo wa Ukraine na kuwekewa vikwazo kwa Urusi kwa kuchochea mzozo huo na hukumu ya kuruhusu matumizi ya bangi kwa wagonjwa nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizohodhi tahariri za magazeti ya Ujerumani Jumatano (23.07.2014).
Gazeti la Thüringische Landeszeitung la mji wa Weimar a linaandika kwamba ule uhuru wa kuandamana,uhuru wa kujieleza au shutuma dhidi ya serikali ya Israel mambo ambayo yanapaswa kuruhusiwa wakati wote imekuwa sio hivyo tena. Chuki dhidi ya Uyahudi inayopaliliwa na watu wachache wenye misimamo mikali sio tu iko nchini Ujerumani bali pia katika nchi nyengine nyingi tena ikiwa katika hali mbaya zaidi kuliko ile ya Ujerumani.Kila mmoja anabidi ashughulikie tatizo lake.Kwa upande wa Ujerumani sio ni kwa sababu ya suala la maangamizi ya Wayahudi yaliyotokea nchini bali pia ni kwa sababu kuheshimu haki za binaadamu ni nguzo muhimu ya mfumo wa kisiasa wa Ujerumani ambao umeamuwa kukomesha chuki za kibaguzi dhidi ya Uyahudi.Jambo hilo halina nafasi tena nchini Ujerumani.
Jumuiya ya kimataifa iwajibike
Gazeti la Main Posts la Würzburg likizungumzia mzozo wa Gaza na chuki iliyoibuwa linasema kwa sasa wachochezi kutoka pande zote mbili ndio wenye usemi kuuzidishia unyama mzozo huo na pia kuzidisha misimamo mikali.
Gazeti hilo linaendelea kusema ufumbuzi wa mataifa mawili, Wapalestina wakiwa na taifa lao wenyewe pembezoni mwa taifa la Kiyahudi ni porojo.Mtaalamu wa Mashariki ya Kati Michael Lüders ana hofia kama matokeo ni kuwepo kwa taifa la Israel litakalokuwa na utawala wa ubaguzi wa rangi ambao Wayahudi wachache watawakandamiza Waarabu walio wengi na hatari ya kuzuka kwa vita vikubwa. Maafa kwa pande zote mbili yanaendelea.Jumuiya ya Kimataifa inatakiwa iwajibike hususan marafiki wa Israel.
Mzozo wa Ukraine wakirihisha
Gazeti la Badische Nachricten la Karslruhe linazungumzia mzozo wa Ukraine katika uhairiri wake ambapo linasema:
Kwa namna Rais Valdimir Putin wa Urusi alivyotowa maelezo kuhusu maafa ya kudunguliwa kwa ndege ya Malaysia huko Ukraine na kwa jinsi waasi walivyozishughulikia maiti za mkasa huo pamoja na vitu vyao ni jambo la kukirihisha. Hata hivyo Umoja wa Ulaya umerudi nyuma katika kuchukuwa hatua muhimu na kwa mara nyengine tena hakutokuwa na vikwazo vya kiuhumi dhidi ya Urusi na Ufaransa tayari imeonyesha haina tatizo kwa hilo inaipatia Urusi helikopta mbili chapa ya Mistral.
Bangi ruksa kwa wagonjwa
Hukumu ya kuruhusu matumizi ya bangi nchini Ujerumani imezungumziwa na magazeti mbali mbali likiwemo la Stuttgarter Nachrichten ambalo linasema hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama ya Cologne ni kama pigo kubwa kwa Taassi ya Shirikisho inayoshughulikia Madawa na Vifaa vya Matibabu na kwa maana hiyo serikali ya Ujerumani.
Gazeti hilo linasema iwapo mgonjwa anaelekezwa kuendelea kutumia bangi kwa kuruhusiwa kuiotesha mwenyewe hapo tena suala linakuwa sio iwapo bali vipi na bora hivyo kwa maslahi ya wagonjwa walio taabani ambapo hakuna kengine kinachoweza kusaidia.
Mwandishi: Mohamed Dahman/Inlandspresse
Mhariri : Josephat Charo