1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bangladesh kuwahamishia Warohingya kisiwa kisichokaliwa

6 Februari 2017

Serikali ya Bangladesh inapanga kuwahamishia katika kisiwa kisichokaliwa, Waislamu wa Rohingya waliotoroka ukandamizaji nchini Myanmar, hatua inayokosolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu na Umoja wa Matifa.

https://p.dw.com/p/2X24P
Rohingya Flee Into Bangladesh As Crisis Deepens
Hivi ndivyo hali ilivyo katika mmoja ya makambi ya wakimbi wa Rohingya katika wilaya ya Cox Bazar nchini Bangladesh.Picha: Getty Images/A. Joyce

Mpango huo umezusha wasiwasi miongoni mwa Warohingya na baadhi ya makundi ya haki za binadamu, huku Umoja wa Mataifa ukielezea wasiwasi kutokana na mazingira ya kijiografia ya eneo hilo.

Waziri wa mambo ya nje wa Bangladesh Mahmood Ali aliwaarifu juu ya mpango huo, wanadiplomasia na wawakilioshi wa mashirika wapatao 60 yakiwemo ya Umoja wa Mataifa, na kuomba msaada wao katika kuwahamisha Warohingya hao kutoka kambi zilizofurika katika wilaya ya Cox Bazar kwenda kisiwa cha Thengar Char kilichoko kusini-mashariki mwa Bangladesh. Maafisa wa serikali wamesema tayari serikali inapima eneo hilo.

Kambi Bangladesh zaelemewa

Zaidi ya Warohingya 300,000 wamekuwa wakiishi nchini Bangladesh kwa miongo kadhaa wakati wengine 66,000 wamevuka mpaka tangu Oktoba, kufuatia ukandamizaji mbaya wa vikosi vya usalama vya Myanmar, na mashambulizi ya kuwalenga yanayofanywa na wanajeshi na waumini wa madhehebu ya Budha walio wengi katika jimbo la Rakhine.

Rohingya Flüchtlinge in Bangladesh
Wakimbizi wa Rohingya wakisubiri kuingia katika kambi ya Kutupalang katika wilaya ya Cox Bazar nchini Bangladesh.Picha: Reuters/M. P. Hossain

Warohingya waliotoroka hivi karibuni wamesema wanajeshi na Wabudha wamechoma makaazi yao, kuwabaka wanawake na kuwauwa Warohingya, baada ya watu ambao hawakutambuliwa kuuwa askari tisa wa mpakani nchini Myanmar. Vurugu hizo zilisababisha ukosoaji wa kimataifa dhidi ya Myanmar, huku Bangladesh ikihangaika kuwahifadhi Warohingya waliovuka mpaka.

Waziri Ali aliwaambia wanadiplomasia kwamba idadi kubwa ya wakimbizi inafanya iwe vigumu kwa serikali kutoa msaada wa kutosha, na imesababisha matatizo ya kijamii, kiuchumi, kimazingira na kiusalama. Kisiwa cha Thengar Char ndiyo mlango wa Mto Meghna na kilitoka baharini miaka minane tu iliopita, na hufurika kila inapotokea dhoruba kubwa.

Wataka kurudi kwao Myanmar

Badala ya kupelekwa kiswani huko, Warohingya wameiomba jamii ya kimataifa kuwasaidia kuishinikiza serikali ya Myanmar iwarejeshee uraia wao. "Hatutaki kuishi Bangladesh kwa muda mrefu, tunataka kurudi nchini kwetu Myanmar, lakini serikali ya Burmer ilifuta uraia wetu, hivyo tunauomba Umoja wa Mataifa utusaidie kuishinikiza serikali hiyo ili turejeshewe uraia wetu," alisema Mohammad Younus mmoja wa wakimbizi hao.

"Na wakati tunapoendelea kuishi Bangladesh, tunaomba tutendewe kama binadamu ili tupate makaazi mazuri, chakula, matibabu yanayostahiki na elimu. Tunataka kujenga jamii ilioelimika na tunaomba jamii ya kimataifa itusaidie." Makundi ya haki za binaadamu na Umoja wa Mataifa yamekosoa mpango huo wa serikali ya Bangladesh.

Indonesien Protest gegen Gewalt an Rohingya Angehörigen in Myanmar
Waandamanaji wakipaza sauti kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuwanusuru Waislamu wa Rohingya wanaokabiliwa na mateso nchini Myanmar.Picha: Getty Images/AFP/B. Ismoyo

Jeshi, polisi watuhumiwa kubaka

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Huma Rights Watch limesema katika ripoti yake iliotolewa jumatatu kwamba jeshi la Myanmar na walinzi wa mpakani walishiriki katika ubakaji wa kimakundi na mashambulizi ya kingono katika vijiji visivyopungua tisa katika wilaya ya Maungdaw kuanzia Oktoba 9 hadi katikati mwa Desemba.

Shirika hilo lenye makao yake mjini New York Marekani, lilisema wasichana wa hadi miaka 13 walibakwa katika kampeni ya maksudi ya wanajeshi na askari polisi, baada ya kukusanya ushahidi kutoka kuhusu matukio 28 tofauti ya mashambulizi ya kingono, ikiwemo mahojiano na wanawake tisa waliosema kuwa walibakwa, au kubakwa kimakundi kwa mtutu wa bunduki na vikosi vya usalama wakati wa kile kinachoitwa "operesheni safisha" kaskazini mwa jimbo la Rakhine.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,ape

Mhariri: Grace Patricia Kabogo