1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBangladesh

Bangladesh yapiga marufuku maandamano

19 Julai 2024

Maandamano ya wanafunzi ya kupinga mgao wa nafasi za kazi za serikali yanayoendelea nchini Bangladesh yamesababisha uharibifu mkubwa wa majengo ya serikali na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kote nchini humo.

https://p.dw.com/p/4iVVa
Bangladesch
Polisi wakikabiliana na waandamanaji katika eneo la Rampura mjini DhakaPicha: Mohammad Ponir Hossain/REUTERS

Machafuko ya wiki hii yamesababisha vifo vya takriban watu 39, wakiwemo watu 32 waliouawa jana Alhamisi, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka baada ya ripoti za mapigano katika karibu nusu ya wilaya 64 za nchi hiyo.

Wanafunzi wameingia barabani tena leo Ijumaa asubuhi kabla ya kuanza maandamano yanayotarajiwa kufanyika baada ya sala ya Ijumaa katika taifa hilo lenye Waislamu wengi.

Soma pia: Banghladesh yamuachia huru kiongozi wa chama cha kiislamu

Bidisha Rimjhim, ni mmoja wa mwanafunzi waliojitokeza kwenye maandamano hayo:

"Tunataka haki itendeke kwa ndugu zetu waliouawa, tunachotaka kwanza ni waziri mkuu lazima atuombe radhi kwa maneno yake machafu. Inakuwaje mkuu wa serikali atoe maneno yasoyofaa kuhusu wanafunzi, atuombe radhi, pili. sheria lazima zichukuliwe kwa ajili ya ndugu zetu waliouawa."

Marufuku ya maandamano

Bangladesch | Maandamano ya Dhaka
Walinzi wa Mpaka wa Bangladesh (BGB) wakilinda Chuo Kikuu cha Dhaka katika mji mkuu mnamo Julai 17, 2024 huku kukiwa na maandamano ya wanafunzi.Picha: MUNIR UZ ZAMAN/AFP

Jeshi la polisi la Dhaka lilichukua hatua kali ya kupiga marufuku mikusanyiko yote ya watu kwa mara ya kwanza tangu maandamano yaanze katika juhudi za kuepusha siku nyingine ya ghasia.

Taarifa iliyotolewa na polisi imesema kuwa waandamanaji wamechoma, kuharibu na kutekeleza  uharibifu kwenye ofisi nyingi za polisi na serikali, ikiwa ni pamoja na ni makao makuu ya shirika la utangazaji la Bangladesh, Televisheni ya Dhaka, ambayo hadi sasa bado haiko hewani baada ya mamia ya wanafunzi waliojawa na hasira kuvamia jumba hilo na kuliteketezeza kwa moto.

Msemaji wa Polisi wa Dhaka Faruk Hossain amesema maafisa wamemkamata Ruhul Kabir Rizvi Ahmed, katibu mwenza wa chama kikuu cha upinzani cha Bangladesh Nationalist Party (BNP) kwa madai kwamba "anakabiliwa na mamia ya kesi," bila kutoa maelezo zaidi.

Shirika la utangazaji la Independent Televisheni liliripoti, Takriban wilaya 26 kote nchini zilishuhudia mapigano siku ya Alhamisi. Mtandao huo umesema zaidi ya watu 700 wamejeruhiwa kwa siku nzima wakiwemo askari polisi 104 na waandishi wa habari 30.

Waandamanaji waongeza shinikizo

Bangladesh | Dhaka
Makabiliano kati ya waandamanaji na wanafunzi nchini BangladeshPicha: Mohammad Ponir Hossain/REUTERS

Wanafunzi hao wanataka kukomeshwa kwa mfumo wa ajira serikalini ambao wanasema unayapendelea makundi maalum ikiwemo watoto wa vigogo.

Serikali ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina, inashutumiwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kutumia vibaya taasisi za serikali kujikita kwenye mamlaka na kukomesha upinzani, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela ya wanaharakati wa upinzani.

Soma pia: Sheikh Hassina ashinda muhula wa tano Bangladesh

Wanafunzi wameapa kuendeleza kampeni zao licha ya Hasina kutoa hotuba ya kitaifa kwenye kituo cha utangazaji cha serikali ambacho sasa hakipo mtandaoni akitaka kutuliza ghasia hizo.