Baraza kuu lapiga kura dhidi ya hatua ya Trump Jerusalem
22 Desemba 2017Zaidi ya nchi 120 zimekaidi kauli ya rais Donald Trump wa Marekani jana Alhamis na kupiga kura kuunga mkono azimio la baraza kuu la Umoja wa Mataifa linalotoa wito kwa Marekani kuachana na hatua yake ya hivi karibuni kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel.
Trump alitishia kupunguza misaada ya kifedha kwa nchi ambazo zitapiga kura kuunga mkono azimio hilo. Jumla ya nchi 128 ziliunga mkono azimio hilo, ambalo halilazimishi kisheria, nchi tisa zilipiga , na 35 zilijizuwia kupiga kura. Nchi 21 hazikupiga kura.
Kitisho cha Trump kinaonekana kuleta athari kwa kiasi fulani , ambapo nchi nyingi zilijizuwia kupiga kura na kupuuzia azimio hilo ambalo kwa kawaida huhusiana na maazimio yanayoihusu Palestina.
Pamoja na hayo, Marekani imejikuta ikitengwa wakati nchi nyingi za magharibi pamoja na washirika wake katika mataifa ya Kiarabu yalipiga kura kuunga mkono azimio hilo. Baadhi ya washirika hao , kama Misri, Jordan na Iraq, wanapokea misaada mikubwa ya kijeshi ama kiuchumi kutoka Marekani, licha ya kuwa kitisho cha Marekani kupunguza misaada hakikulengwa kwa nchi yoyote maalum.
Kwa Wapalestina ni ushindi
Msemaji wa rais Mahmoud Abbas wa Palestina inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi aliita kura hiyo "ushindi kwa Palestina." Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameipinga kura hiyo.
Mapema mwezi huu , Trump alibadilisha sera ya miongo kadhaa ya Marekani kwa kutangaza Marekani kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel. Mji ambao ni eneo takatifu kwa Waislamu, Wayahudi na Wakristo, na kwamba Marekani itahamishia ubalozi wake katika mji huo.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley ameliambia baraza kuu la Umoja wa Mataifa kabla ya kura ya jana kwamba "Marekani itaikumbuka siku hii ambapo imeshambuliwa katika baraza kuu kwa ukweli kwamba inatekeleza haki yake kama taifa.
"Tutaikumbuka wakati tutakapotakiwa kwa mara nyingine tena kutoa mchango mkubwa kabisa kwa ajili ya Umoja wa Mataifa, na mataifa mengi yanakuja kwetu kutuomba , kama wanavyofanya kila mara , kuchangia zaidi na kutumia ushawishi wetu kwa faida yao," amesema balozi huyo.
Kikwazo cha amani
Hadhi ya mji wa Jerusalem ni kikwazo kikubwa kwa makubaliano ya amani kati ya Israel na Palestina, ambao walikasirishwa na hatua ya Trump.
Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa mataifa Francois Delattre amesema katika taarifa : "Azimio hili lililoidhinishwa leo linathibitisha tu uhalali wa sheria ya kimataifa kuhusu Jerusalem." Ufaransa ilipiga kura kuunga mkono azimio hilo.
Baadaye jana Alhamis , balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley ameyataka mataifa 64 yaliyopiga kura ya hapana, kujizuwia ama kutopiga kura kabisa kufika katika ghafla Januari 3 "kuwashukuru kwa urafiki wenu kwa Marekani."
Mwanidshi: Sekione Kitojo /Sylvia mwehozi
Mhariri: Saumu Yusuf