1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la juu Uingereza larekebisha mswada wa Brexit

Yusra Buwayhid
2 Machi 2017

Baraza la juu la bunge la Uingereza (House of Lords) limepiga kura ya kutaka mswada wa wa Brexit ufanyiwe marekebisho. Marekebisho hayo yanasisitiza kulinda haki za raia wa Ulaya wanaoishi nchini humo.

https://p.dw.com/p/2YVNg
UK | House of Lords
Picha: picture-alliance/empics/PA

Marekebisho yanayotaka raia wa nchi za Umoja wa Ulaya wanaoishi Uingereza kwa sasa waendelee kuwa na haki kama walizokuwa nazo wakati Uingereza ikiwa mwanachama wa umoja huo, yalipitishwa katika baraza hilo kwa kura 358 dhidi ya 256.

Hata hivyo mabadiliko hayo huenda yakachelewesha mswada unaompa mamlaka Waziri Mkuu Theresa May kuanzisha kipengele cha 50 cha Mkataba wa Lisbon cha kuanzisha mchakato wa kujiengua kutoka Umoja wa Ulaya. May amesema amepanga kuanzisha rasmi mchakato huo mwisho wa Machi.

Uamuzi wa Uingereza kujiondoka katika Umoja wa Ulaya ulitokana na kura ya maoni ya mwezi Juni mwaka jana. Asiliamia 52 ya wananchi walipiga kura ya ndio ya kutaka nchi yao ijitoe katika umoja huo.

Kabla ya kura hiyo ya baraza la juu iliyofanyika jana, May alisema ratiba yake ya kuanzisha ibara ya 50 haitobadilika.

 "Nadhani atazingatia wanachokisema, lakini nina hakika serikali itawapinga,” amesema mjumbe wa baraza hilo, Bwana Norman Lamont.

Msemaji wa serikali ya May amesema serikali imesikitishwa kuwa baraza  la juu linataka mswada uliopitishwa na Bunge la Uingereza ufanyiwe marekebisho.

Raia wa Ulaya wanahitaji kujua haki zao

Kwa upande mwengine, msemaji mkuu wa chama cha Labour, Dianne Hayter, amesema marekebisho hayo ni muhimu kwasababu raia wa bara la Ulaya wanaoishi Uingereza wanahitaji kujua haki zao hivi sasa, sio baada ya miaka miwili au hata mwaka mmoja.

Theresa May EU Fahne
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: picture-alliance/empics/N. Carson

Licha ya kura iliyopingwa na baraza la juu la bunge la Uingereza House of Lords, lazima sasa mswada huo pamoja na pendekezo hilo, urejeshwe katika bunge - House of Commons, ambapo kuna uwezekano mkubwa wa kukataliwa.

Kwa kujitoa katika Umoja wa Ulaya, Uingereza pia itaepukana na sera ya umoja huo ya uhuru wa kusafiri bila ya kujali mipaka barani humo. Ni sera inayo wawezesha raia wa nchi zote wanachama 28, kuishi na kufanya kazi katika nchi yoyote miongoni mwa hizo.

Matokeo yake, watu wapatao milioni tatu ambao ni raia wa nchi za Ulaya wanaoishi Uingereza, na raia milioni moja wa Kiingereza wanaoishi nchi nyingine barani humo hawana hakika ya hatma ya maisha yao.

Hamna mwenye kujua hatma ya kazi yake au makaazi yake pale Uingereza itakapojiondoa rasmi katika Umoja wa Ulaya na kuanza kudhibiti tena mipaka yake pamoja na uhamiaji.

Serikali ya May imesema itahakikisha haki za raia wa Ulaya wanaoishi Uingereza zinabaki pale plae, ikiwa Waingereza nao wanaoishi nchi za nje barani humo watapatiwa haki hizo hizo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap/dw

Mhariri:Hamidou Oummilkheir