1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Baraza la Katiba Senegal lachapisha orodha mpya ya wagombea

21 Februari 2024

Baraza la Katiba la Senegal limechapisha orodha iliyorekebishwa ya wagombea wa uchaguzi wa rais uliocheleweshwa kutoka Februari 25 hadi tarehe ambayo haijatangazwa

https://p.dw.com/p/4cdYI
Maandamano ya Senegal yalisababisha vifo kadhaa
Makundi ya kiraia na kisiasa Senegal yanataka ratiba ya uchaguzi iheshimiwe na Rais Macky Sall Picha: John Wessels/AFP

Baraza hilo wiki iliyopita lilibatilisha muswada uliochelewesha uchaguzi hadi Desemba na sasa Rais Macky Sall ameahidi kuheshimu uamuzi huo na kufanya mashauriano ya kuandaa uchaguzi huo haraka iwewekanavyo.

Kuondolewa kwa kiongozi wa upinzani Rose Wardini kumepunguza idadi ya wagombea kutoka ya awali 20 hadi 19. Viongozi maarufu wa upinzani, akiwemo mwanasiasa Ousmane Sonko na Karim Wade, mtoto wa rais wa zamani Abdoulaye Wade, bado wamefungiwa kushiriki.

Mashirika ya kiraia nchini humo sasa yanataka uchaguzi ufanyike kabla ya muhula wa rais Macky Sall haujakamilika mwezi Aprili. Wagombea 15 walisaini baruainayotaka tarehe ya uchaguzi na tarehe ya rais Macky Sall Kuachia ngazi zisipindukie Aprili tarehe 2. Barua hiyo imeonekana na shirika la habari la AFP na imethibitishwa. Rais Macky Sall ameshasema kwamba dhamira yake ni kuheshimu uamuzi wa baraza la katiba na atafanya mashauriano yanayohitajika kuandaa uchaguzi huo wa raia mapema iwezekanavyo.

Kufuatia siku kadhaa za maandamano nchini humo serikali yake imeamuwa kuwaachilia huru wafungwa 300 katika kipindi cha saa 48 zilizopita. Wengi walioachiliwa  ni watu waliokuwa wamezuiliwa jela baada ya kukamatwa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano.