1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama kupigia kura azimio la kusaidiwa Gaza

21 Desemba 2023

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linajiandaa kupiga kura leo Alhamisi kuhusu azimio juu ya kupelekwa msaada katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4aS34
UN-Sicherheitsrat | Veto der USA zur Resolution
Picha: CHARLY TRIBALLEAU/AFP/Getty Images

Baraza hilo liliakhirisha mara kadhaa mchakato huo kutokana na msimamo wa Marekani. Mbali na hilo, Israel imeendelea kufanya mashambulio makali  dhidi ya Gaza huku kundi la Hamas nalo likiripotiwa kufyetuwa maroketi dhidi ya Israel.

Azimio jipya la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupigiwa kura (21.12.2023) baada ya kuakhirishwa mara kadhaa, ikielezwa kwamba Marekani na nchi za Kiarabu zimekuwa katika majadiliano ya kidiplomasia kujaribu kuepusha hatua ya kushindwa kupitishwa kwa mara nyingine azimio hilo linalohusu hatua ya kupelekwa msaada kwa watu wa Gaza.

Baraza la usalama lisifanye ''undumilakuwili wa hatari''.

Waziri wa mambo ya nje wa Jordan Ayman Safadi ameonya kwamba ikiwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litashindwa kupitisha azimio hilo kuhusu Gaza itamaanisha linafanya kile alichokiita ''undumilakuwili wa hatari''. Safadi amesema azimio hilo linalenga zaidi hatua ya kuharakishwa usafirishaji wa msaada ambao Israel imetajwa kuuzuia kupelekwa Gaza kuyaokoa maisha ya watu.

Gaza Rauch steigt nach einem israelischen Angriff auf Rafah im südlichen Gazastreifen
Mashambulizi yakiendelea katika eno la Rafah, kusini mwa Ukada wa GazaPicha: Ismael Mohamad/UPI Photo/IMAGO

Vita vya Hamas na Israel vimesababisha mgogoro mbaya wa kibinadamu ndani ya Gaza ambako maelfu ya watu wamesongamana katika makaazi ya muda na mahema yaliyoundwa huko Gaza huku pia wakikabiliana na ukosefu wa chakula, dawa na mahitaji mengine ya msingi. Afisa wa shirika la afya duniani WHO aliyetembelea hospitali mbili za Kaskazini mwa Gaza amesema madaktari wanalazimika kuwakata viungo  wagonjwa wengi  kutokana na upungufu wa madaktari, umeme pamoja na vifaa.

Wakati juhudi za kidiplomasia za kutafuta usitishwaji mapigano kwa mara nyingine pamoja na kupelekwa msaada, zikiendelea, Israel imefanya mashambulizi mengine zaidi dhidi Gaza na operesheni nyingine kote katika eneo hilo. Imekuwa vigumu kuthibitisha kuhusu mapigano hayo kutokana na sehemu kubwa ya Gaza kukosa mawasiliano.

Kundi la Hamas bado linaonekaa bado halijashindwa vita

Lakini imeripotiwa kwamba kundi la Hamas limefyetuwa maroketi kuelekea mji wa Tel Aviv hatua ambayo inaonesha kwamba kundi hilo bado halijakubali kushindwa katika kampeini ya kijeshi ya Israel inayolenga kuliangamiza. Takriban Wapalestina 20,000 wameuwawa tangu Israel ilipotangaza vita dhidi ya Hamas kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza.

Israel imesema zaidi ya wanajeshi wake 130 wameuwawa katika mapambano yake ya ardhini tangu Hamas walipovamia Kusini mwa Israel Oktoba 7 na kuwauwa watu kiasi 1,200 wengi wakiwa ni raia na kuwachukuwa mateka wengine takriban 240.

Hivi sasa Israel inasema imegunduwa kituo cha chini kwa chini cha kuongoza mashambulio cha Hamas katika mji wa Gaza.Israel pia imeshambulia mpakani mwa Lebanon katika mji wa Maroun El-Ras leo Alhamisi na kumuua mwanamke mmoja mzee wa miaka takriban 80 na kumjeruhi mumewe kwa mujibu wa shirika la habari la Lebanon.

Jeshi la Israel limesema lilifyetuwa makombora na kufanya mashambulio ya anga kuzilenga ngome za kundi la Hezbollah Kusini mwa Lebanon jana Jumatano jioni na mapema leo. Wakati huohuo Iraq imesema imesafirisha lita milioni 10 za mafuta kutoka bandari ya Basra  kuelekea Misri kwaajili ya kusaidia kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo kwa watu wa Ukanda wa Gaza. Hapa Ulaya nchini Uholanzi kundi la wafanyakazi wa serikali wamefanya maandamano yasiyo ya kawaida mbele ya wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo leo kushinikiza usitishwaji mapigano katika Gaza.

Soma zaidi:Kiongozi wa Hamas awasili Misri kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza

Wafanyakazi wa wizara takriban 150  walibeba mabango yaliyoandikwa ujumbe unaosema wafanyakazi wa serikali wataka vita visitishwe. Uholanzi kama ilivyo Ujerumani na Italia wiki iliyopita zilijizuia kupiga kura ya kudai vita visitishwe wakati wa mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa,licha ya mataifa mengi ya ulimwengu kuliunga mkono azimio hilo.

Vyanzo: RTR/AFP/AP

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW