Baraza la UN halijaafikiana juu ya Palestina
12 Aprili 2024Baada ya mkutano uliofanyika Alhamisi mjini New York nchini Marekani, balozi wa Malta katika Umoja wa Mataifa Vanessa Frazier ambaye kwasasa ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo ya Baraza la Usalama, alisema kuwa theluthi mbili ya mataifa wanachama wa baraza hilo yaliunga mkono ombi hilo laPalestinala kutaka hadhi ya uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa huku matano yakipinga.
Frazier amesema kuwa atasambaza ripoti kuhusu suala hilo miongoni mwa wanachama wa Baraza la Usalama haraka iwezekanavyo.
Soma pia: Palestina yataka uanachama kamili ndani ya Umoja wa Mataifa
Kamati hiyo inaonekana kutokuwa na uwezekano wa kupendekeza kura ya hoja hiyo katika Baraza la Usalama . Hata hivyo, taifa lolote mwanachama linaweza kuwasilisha azimio sawa na hilo wakati wowote.
Kulingana na duru za kidiplomasia, Algeria inapanga kufanya hivyo katika wiki zijazo.
China inaunga mkono ombi la Palestina
China inaunga mkono unachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa. Wakati wa mkutano na waandishi habari hapo jana mjini Beijing, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa nchi Mao Ning alisema kuwa mzozo unaoendelea kati ya Palestina na Israel na mzozo mkubwa wa kibinadamu uliosababisha ni ukumbusho mwingine kwamba njia pekee ya kumaliza mzunguko mbaya wa migogoro ya Palestina na Israeli ni kutekeleza kikamilifu suluhisho la mataifa mawili, kuanzisha taifa huru la Palestina na kurekebisha dhuluma ya kihistoria ya muda mrefu kwa Wapalestina.
Ning ameongeza kuwa China inaunga mkono uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa kwa Palestina na inaunga mkono hatua za haraka za Baraza hilo kufanikisha hilo.
Kwa hoja hiyo ya Palestina kufanikiwa, angalau wanachama tisa wa Baraza la Usalama watapaswa kuiunga mkono na kutopingwa na mwanachama yoyote wa kudumu katika baraza hilo kama vile China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani.
Blinken aitaka China kuizuia Iran kutoishambulia Israel
Wakati wa mazungumzo kwa njia ya simu kati ya waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi na mwenzake wa Marekani Antony Blinken, Blinken aliitaka China kutumia ushawishi wake kuizuia Iran kutoishambulia Israel. Haya ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani.
Soma pia: Kiongozi mkuu wa Iran aapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel
Hii ni baada ya kuongezeka kwa wasiwasi wa mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran baada ya shambulizi la Israel dhidi ya ubalozi wake mdogo mjini Damascus nchini Syria mnamo Aprili 1.
China yalaani shambulizi la Israel dhidi ya ubalozi wa Iran nchini Syria
Wang ameeleza ghadhabu ya China juu ya shambulizi hilo huku akisisitiza kuhusu haki isiyoweza kukiukwa ya usalama wa taasisi za kidiplomasia na haja ya kuheshimu uhuru wa Iran na Syria.
Vikosi ya Israel vyawauwa Wapalestina wawili
Vikosi vya Israel vimewaua kwa kuwapiga risasi Wapalestina wawili katika uvamizi uliofanyika mapema leo karibu na mji wa Tubas katika eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu. Haya yameripotiwa na shirika la habari laPalestina Wafa.
Jeshi la Israel halikutoa tamko la haraka kuhusu shambulizi hilo.
afp,dpa