1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama latafakari kutuma jeshi zaidi Sudan Kusini

24 Desemba 2013

Takriban raia 45,000 wa Sudan Kusini wamekimbilia kutafuta hifadhi katika kambi za Umoja wa Mataifa kufuatia mapigano makali yanayoendelea kushuhudiwa kuenea katika taifa hilo changa.

https://p.dw.com/p/1AgGa
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New YorkPicha: Reuters

Idadi rasmi iliyotangazwa na serikali ya watu waliouwawa imefikia watu 500 ingawa inaaminika kuwa ni zaidi huku ikiarifiwa kiasi nusu ya majimbo 10 ya taifa hilo yamekumbwa na vita hivyo. Watu wasiopungua 20,000 wamekimbilia usalama katika kambi mbili za Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Juba wakati wengine 17,000 wametafuta hifadhi katika kambi nyingine ya Umoja huo wa Mataifa katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Bor mji mkuu wa jimbo la Jonglei mashariki ya Sudan Kusini.

Katibu mkuu wa UN Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa UN Ban Ki MoonPicha: picture alliance/abaca

Halikadhalika kuna watu 7,000 wanaojihifadhi katika kambi ya Umoja huo kwenye jimbo la Bentiu mji mkuu wa jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Unity na ambalo pia liko mikononi mwa waasi.Umoja wa Mataifa ukitowa taarifa hiyo pia umeongeza kusema kwamba kuna mapigano makali yaliyoripotiwa kuzuka katika eneo la Upper Nile jimbo jingine lenye mafuta mengi.

Kwa ujumla Umoja huo unasema kuna watu 45,000 waliokimbilia hifadhi katika makambi yake mbali mbali katika taifa hilo la Sudan Kusini.Shirika la Umoja huo linalohusika na uratibu wa masuala ya kiutu OCHA,limesema idadi ya watu walioachwa bila makaazi kufuatia mzozo huu mpya inakadiriwa kufikia watu 81,000 na pengine zaidi ya hiyo.

Raia waliokimbilia kambi za Umoja wa Mataifa mjini Juba
Raia waliokimbilia kambi za Umoja wa Mataifa mjini JubaPicha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Mataifa pia unasema kuna taarifa za kuthibitika kwamba mateso makubwa na uvunjaji wa haki za binadamu umefanywa dhidi ya raia katika sehemu mbali mbali za taifa hilo ikiwemo mauaji. Hali ya wasiwasi mkubwa iko katika mji wa Bor,mji ulioko kilomita 200 kutoka Kaskazini mwa Juba ambako jeshi limesema linajiandaa kufanya operesheni kubwa ya kuukombowa mji huo tangu baada ya kutwaliwa na waasi siku ya Jumatano.

Aidha hali inatajwa kuwa ngumu zaidi katika kambi inayowahifadhi raia katika mji huo kukishuhudiwa changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa chakula na malazi.Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameliomba baraza la usalama la Umoja huo kutuma wanajeshi 5,500 zaidi wa kulinda amani haraka iwezekanavyo ili kuwalinda raia nchini humo.

Mjumbe maalum wa Marekani Sudan Kusini Donald Booth
Mjumbe maalum wa Marekani Sudan Kusini Donald BoothPicha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Baraza hilo lenye wanachama 15 limekutana kujadili mzozo huo na linatarajiwa leo hii kupigia kura azimio la kuongeza wanajeshi wa kulinda amani katika nchi hiyo.Kwa upande mwingine viongozi wanaoonyeshana ubabe uliosababisha vurugu hizo ,Kiongozi wa waasi Riek Machar na rais Salva Kiir wameashiria kuwa tayari kuzungumza kujaribu kuumaliza mgogoro huo uliokwisha sababisha mauaji ya mamia ya watu.

Hata hivyo afisa mmoja kutoka serikalini amesefahamisha kwamba Sudan Kusini haiwezi kuridhia pendekezo la Machar la kutaka viongozi wa upinzani waliokamatwa waachiwe huru.Inaarifiwa tayari mjumbe maalum wa Marekani katika Sudan Kusini Donald Booth alikutana na viongozi hao wapinzani waliokamatwa na kuzungumza nao ambapo walielezea bayana utayarifu wao wa kuumaliza mzozo huu kupitia mdahalo na maridhiano.Booth pia alikutana jana na rais Kirr aliyesema yuko tayari kuzungumza na Machar.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman