1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la waasi wa Libya lakutana na wajumbe wa kimataifa

Abdu Said Mtullya13 Aprili 2011

Baraza la Kitaifa la waasi wa Libya lawania kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa

https://p.dw.com/p/10sCF
Waziri wa mambo ya je wa Ujerumani Guido Westerwelle atahudhuria mkutano na wawakilishi wa Baraza la waasi wa Libya mjini DohaPicha: picture-alliance/dpa

Wajumbe wa Baraza la Kitaifa la waasi wa Libya leo wanakutana na wawakilishi wa kimataifa mjini Doha kuzungumzia juu ya kutambuliwa kwa Baraza hilo. Msemaji wa Baraza hilo ameeleza kuwa waasi wanatumai kutambuliwa ,hatua kwa hatua, kuwa wawakilishi halali wa Libya.Mpaka sasa Baraza la kitaifa linalowawakilisha waasi wa Libya linatambuliwa na Ufaransa,Italia na Qatari tu.

Jopo la kimataifa linalowasiliana na waasi wa Libya lililoundwa mjini London wiki mbili zilizopita, kwa mara ya kwanza litatafakari njia za kuleta amani nchini Libya.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle pia atahudhuria mkutano huo wa mjini Doha. Wengine watakaohudhuria ni wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya,Umoja wa Mataifa,Marekani na kutoka Umoja wa nchi za Kiarabu.

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya umeimarisha vikwazo dhidi ya utawala wa Kanali Gaddafi.Nchi za Umoja wa Ulaya zitazizuia akaunti za benki za makampuni 26 ya Libya na zitayapiga marufuku makampuni ya nchi za Umoja huo kufanya biashara na makampuni ya Libya.