1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona na Real Madrid zahitaji muujiza

29 Aprili 2013

Mahasimu wawili wakali Barcelona na Real Madrid kwa mara ya kwanza watakuwa na lengo la pamoja baada ya vichapo vya mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Champions League: Haja ya kuamini katika miujiza

https://p.dw.com/p/18P66
(L-R) Barcelona's Argentinian forward Lionel Messi vies with Bayern Munich's defender Jerome Boateng and Bayern Munich's Brazilian defender Dante during UEFA champions league semi final first leg football match between Bayern Muenchen and FC Barcelona on April 23, 2013 in Munich. AFP PHOTO / ODD ANDERSEN (Photo credit should read ODD ANDERSEN/AFP/Getty Images)
Champions League 2012/13 Halbfinale FC Bayern München FC BarcelonaPicha: ODD ANDERSEN/AFP/Getty Images

Barcelona ina kibarua kigumu cha kuyageuza matokeo ya kichapo cha mabao manne kwa sifuri walichopata kutoka mikononi mwa Bayern Munich watakati timu hizo mbili zitakapokutana kwa mkondo wa pili Jumatano wiki hii, wakati nao Real Madrid kesho Jumanne wakiwa na kibarua kingine cha kutoka nyuma kutokana na kipigo walichopata cha mabao manne kwa moja nyumbani kwa Borussia Dortmund.

Hakuna timu iliyowahi kutoka nyuma na kushinda mchuano wa matokeo ya aina hiyo katika awamu hii ya kinyang'anyiro hicho, jambo linalomaanisha kuwa Finali ya Mei 25 uwanjani Wembley huenda ikazileta pamoja timu mbili za Ujerumani, katika dimba ambalo wajerumani wanalitambua kama “Der Klassiker”.

Mkufunzi wa Real Madrid Jose Mourinho anasema anapaswa kulaumiwa kama watashindwa na Dortmund
Mkufunzi wa Real Madrid Jose Mourinho anasema anapaswa kulaumiwa kama watashindwa na DortmundPicha: Reuters

Baada ya kuzidiwa nguvu na timu hizo mbili za Ujerumani, miamba hiyo ya soka Uhispania itayaweka matumaini yao kwa washambuliaji wawili bora zaidi ulimwenguni. Lionel Messi wa Barcelona amefunga mabao manane katika dimba hili msimu huu wakati naye mwenzake wa Madrid Cristiano Ronaldo, akiongoza kwa kufunga magoli mengi katika kinyang'anyiro hiki akifuatwa na mshambulizi wa Borussia Dortmund Robert Lewandowski. Tatizo kubwa hata hivyo ni kwamba Messi na Ronaldo huenda wasiwe katika hali nzuri kabisa. Wakufunzi wao hata hivyo wamesema kuwa nyota hao wawili watashirikishwa katika vikosi vyao vitakavyoanza kesho na Jumanne.

Bayern yaweka rekodi zaidi katika Bundesliga

Mabingwa wa msimu huu Bayern Munich, walisajili ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Freiburg na kuweka rekodi nyingine ya kukusanya pointi 84 zaidi ya rekodi iliyowekwa na washindi wa msimu uliopita Borussia Dortmund. Dortmund nao ambao wako katika nafasi ya pili kwenye ligi, walipata ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Fortuna Düsseldorf kwa usaidizi wa bao safi lake Nuri Sahin. Werder Bremen walikaribia eneo hatari baada ya kushindwa bao moja kwa sifuri kufuatia penalti yenye utata waliyopewa nambari tatu Bayer Leverkusen, na kuwawacha wakiwa na pointi mbili pekee juu ya eneo la kushushwa daraja baada ya Augsburg kuizaba VfB Stuttgart mabao matatu kwa sifuri.

Ushindi wa Augsburg ulikuwa na maana kuwa washika mkia Greuther Fürth ambao waliingia katika Bundesliga msimu huu, wamerudishwa katika daraja ya pili. Fürth walishindwa mabao matatu kwa mawili na Hanover 96. Bayern na Dortmund zilifanya mabadiliko kumi katika vikosi vyao vilivyoshinda mechi za mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Champions League wiki iliyopita.

Mshambuliaji wa Schalke Klaas-Jan Huntelaar arejea kwa kishindo baada ya kupona jeraha
Mshambuliaji wa Schalke Klaas-Jan Huntelaar arejea kwa kishindo baada ya kupona jerahaPicha: picture-alliance/dpa

Baada ya kushindwa mabao mawili kwa moja na Dortmund, Fortnuna sasa wako katika nafasi nne kutoka nyuma na pointi 30 mbele ya Augsburg na faida ya magoli. Nambari mbili kutoka nyuma Hoffenheim iliipiku Nuremberg mbili kwa moja na kubakia nyuma ya Augsburg na pengo la pointi tatu. VfL Wolfsburg iliwachabanga Borussia Moenchendladbach mabao matatu kwa moja.

Kwingineko Klaas-Jan Huntelaar alibusu wavu mara mbili na kuandaa pasi ya goli jingine wakati aliporudi kutoka mkekani na kuiongoza Schalke kwa ushindi wa mabao manne kwa moja dhidi ya Hamburger SV na kusalia katika nafasi ya nne. Huntelaar hakuwa amecheza kwa wiki sita tangu alipojeruhiwa goti katika mchuano wa utani wa jimbo la Ruhr dhidi ya Borussia Dortmund.

Huku zikiwa zimesalia mechi tatu msimu kukamilika, Schalke wana pointi tatu mbele ya Entracht Frankfurt katika nafasi ya kufuzu katika Champions League. Hii ni baada ya Frankfurt kutoka sare ya bila kufungana goli na Mainz 05. sasa wako katika nafasi ya tano kwenye ligi na pointi 46. Mainz sasa wameteremka hadi nafasi ya kumi na pointi 40, ikiwa ni upungufu wa pointi tano kutoka eneo la kufuzu katika mechi za Europa League.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/Reuters

Mhariri: Abdul-Rahman, Mohammed